Na Mwandishi Maalumu – Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa wizara hiyo kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya kansa yanayoweza kutibika kama yakigundulika mapema.
Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo leo wakati wa zoezi la upimaji wa magonjwa ya Saratani na yasiyo ya kuambukiza linalofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa watumishi wa ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma.
Mhe. Kikwete alisema zoezi hilo ni fursa muhimu kwa watumishi hao kujua hali zao za afya huku akibainisha kuwa wengi wao hukosa muda wa kwenda kupima kutokana na majukumu ya kazi.
“Leo hii wataalamu kutoka Hospitali ya Ocean Road wamekuja hapa kutupima magonjwa ya saratani na yasiyo ya kuambukiza. Ni muhimu kutumia fursa hii kupima afya kwani ukigundulika na changamoto yoyote mapema utaweza kupata matibabu kwa wakati”, alisisitiza.
Mhe. Kikwete aliwashukuru wataalamu wa ORCI kwa kuwafikia watumishi mahali pa kazi hatua hiyo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi na wafanyakazi wake popote walipo.
Alitoa wito kwa taasisi hiyo kuendelea kusambaza huduma hizo katika maeneo mengine ikiwemo ngazi za wilaya ili kuwafikia watumishi wengi zaidi ambao muda mwingi hutumia kazini na kukosa nafasi ya kwenda hospitali kupima afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Diwani Msemo alisema taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma za uchunguzi wa afya katika maeneo mbalimbali nchini ambapo hadi sasa imefikia mikoa 15 na kuhudumia zaidi ya watu 200,000 kupitia programu ya Huduma Mkoba.
Dkt. Msemo ambaye pia ni Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Saratani alieleza kuwa huduma zinazowafuata watumishi mahali pa kazi zimekuwa na mwitikio mkubwa akibainisha kuwa katika ofisi hiyo kwa mud awa siku tatu wamefanikiwa kupima takribani watumishi 200.
Aliongeza kuwa kuchelewa kugundua magonjwa kama Saratani kunafanya matibabu kuwa magumu zaidi hivyo kusisitiza umuhimu wa watu kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.
Nao baadhi ya watumishi waliopata huduma za uchunguzi wa afya waliushukuru uongozi wa Ofisi hiyo kwa kuwaletea huduma za uchunguzi wa afya mahali walipo na kueleza kuridhishwa na zoezi hilo huku wakisema limewasaidia kutambua hali zao za afya na kuchukua hatua stahiki.
Deus Kimaro alisema huduma hiyo imewapa urahisi wa kupima afya bila kuathiri majukumu yao ya kazi kwani siku ya Jumatatu walipata mafunzo ya Saratani na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yaliyokwenda sambamba na huduma ya upimaji ambayo inafanyika kwa muda wa siku tano.
“Huduma zilizotolewa ni bora na zimetupa fursa ya kujua hali zetu za afya mapema, watumishi wengi wamejitokeza kupima tunaomba huduma hizi ziendelee kusambazwa zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuwafikia watu wengi zaidi”, alisema Hawa Mgong’oli Afisa Utawala Mkuu.
Zoezi hilo linaendelea kuwa sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha watumishi wa umma wanakuwa na afya bora hali itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya taifa.






