Na Mwandishi Wetu, JmahuriMedia, Dar es Salaam

Tanzania inatarajiwa kuingiza zaidi ya Sh bilioni 10 kutokana na mauzo ya biashara ya kaboni baada ya Serikali kuidhinisha miradi minne itakayouza tani milioni 4.2 za kaboni katika soko rasmi la kimataifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Agosti 5, 2026.

Ameitaja miradi iliyopata kibali ni nishati safi ya kupikia unaotekelezwa na Burn Manufacturing, programu ya athari za kijamii inayosimamiwa na AP Energy Group kwa kushirikiana na Sayari SA Limited, mradi wa maji safi wa Water Mission International Tanzania na mradi wa majiko banifu unaotekelezwa na Bridge Carbon Tanzania Limited.

Waziri Masauni, miradi hiyo itachangia kupunguza uzalishaji wa gesi joto kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama, kutengeneza ajira na kusaidia utekelezaji wa lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 85 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Amesema mapato hayo yanatokana na asilimia nane ambayo Serikali hupata kutokana na mauzo ya kaboni kwa mujibu wa Kanuni za Usimamizi wa Biashara ya Kaboni.

Amesema tani milioni 4.2 za kaboni zilizothibitishwa zina thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 52.1, sawa na takribani Sh bilioni 135.5, huku Serikali ikitarajia kupata zaidi ya dola za Marekani milioni mbili, sawa na zaidi ya Sh bilioni 10.

“Fedha hizi zinatokana na juhudi za Serikali za kujenga mfumo imara wa biashara ya kaboni unaolinda maslahi ya taifa na kuongeza mchango wa sekta hii katika uchumi,” alisema Masauni.

Amesema Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria, kisera na kitaasisi ili kuhakikisha biashara ya kaboni inafanyika kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania.

Waziri Masauni amesema kupitia marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191, Serikali ilianzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Biashara ya Kaboni (NCMC), ambacho kinasimamia usajili wa miradi, ufuatiliaji, uhakiki, utoaji wa taarifa na uratibu wa mapato yatokanayo na biashara hiyo.

Amesema hadi Julai mwaka huu, NCMC ilikuwa imesajili miradi 117 ya biashara ya kaboni, huku Kamati ya Taifa ya Tathmini ya Miradi ikifanya uchambuzi wa kitaalamu kabla ya kuishauri Serikali kuhusu miradi inayostahili kuidhinishwa.

Amesema Serikali itaendelea kutathmini miradi mingine katika sekta za maji, bioanuwai, usafiri na magari ya umeme ili kuongeza fursa za biashara ya kaboni na kuiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na soko hilo duniani.

Aidha, mradi wa maji ambao utatekelezwa katika Mikoa yote 26 Nchini, inatoa ajira kwa watanzania 1000, za mtu mmoja mmoja na kwa wasambazaji zaidi ya 100. Pia miradi hii inachangia katika juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama katika mkoa wa Kigoma na Dodoma ikinufaisha kaya zaidi ya milioni moja kwa maji safi na kutoa ajira zaidi ya 350 kwa watanzania.