Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Wakulima nchini wametakiwa kuongeza matumizi ya mbolea, viuatilifu na mbegu za asili kama njia ya kuongeza tija ya uzalishaji, kupunguza gharama za kilimo na kulinda afya ya walaji pamoja na mazingira, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuimarisha kilimo ikolojia hai.
Wito huo umetolewa na wadau wa sekta ya kilimo wakati wa mjadala kuhusu pembejeo za kilimo ikolojia hai uliofanyika katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea Dodoma, ambapo inaelezwa kuwa matumizi ya pembejeo rafiki kwa mazingira ni miongoni mwa suluhisho la kukabiliana na changamoto za uchakavu wa udongo, mabadiliko ya tabianchi na gharama kubwa za uzalishaji zinazowakabili wakulima.
Mratibu wa Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO), Abdallah Ramadhan Mkindi, amesema kilimo ikolojia hai si mbadala wa uzalishaji pekee, bali ni mfumo unaoweka uwiano kati ya uzalishaji wa mazao, afya ya binadamu, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa uchumi wa mkulima.
Amesema matumizi yasiyo sahihi ya kemikali yameendelea kuzua wasiwasi kutokana na tafiti mbalimbali kuonyesha uwezekano wa kuathiri afya ya binadamu na kuchafua udongo pamoja na vyanzo vya maji, hivyo kuna umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya pembejeo za asili zinazozalisha chakula salama na kuhifadhi rutuba ya ardhi kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Mratibu Mwandamizi wa Programu wa CSWED Tanzania, Gladness Martini, amesema tafiti shirikishi zimeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuwawezesha wakulima kutambua, kuzalisha na kuhifadhi mbegu za asili zenye ubora na zinazokidhi mazingira ya maeneo mbalimbali.
Amesema ushiriki wa wakulima katika mchakato wa utafiti unawawezesha kuelewa teknolojia mpya za kilimo na kuzitumia kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato.
“Tunawajengea uwezo wakulima kutumia mbinu rafiki kwa mazingira ili wazalishe chakula salama, walinde afya zao na za walaji, huku wakihifadhi rutuba ya ardhi kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema
Kwa upande wake, Meneja wa Usajili na Leseni wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Mwahija Irika, amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia Sheria ya Mbolea, hatua iliyochochea ukuaji wa sekta ya uzalishaji wa mbolea za asili nchini.
Amesema hadi sasa TFRA imesajili zaidi ya aina 65 za mbolea za asili na wazalishaji 15 wanaendelea kuzalisha mbolea hizo nchini, jambo linaloashiria kuongezeka kwa uwekezaji na upatikanaji wa pembejeo zinazounga mkono kilimo endelevu.
“Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na tunashuhudia kampuni mbalimbali zikiingia katika uzalishaji wa mbolea za asili. Wakati huo huo tunaendelea kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea hizo ili kuongeza tija ya uzalishaji na kulinda afya ya udongo,” alisema Irika.
Amefafanua kuwa matumizi ya mbolea za asili huchangia kurejesha na kuhifadhi rutuba ya udongo kwa muda mrefu, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza upatikanaji wa mazao yenye ubora na usalama kwa walaji.
Aidha, amesema Serikali imeweka utaratibu wa kufanya tathmini ya ubora, usalama na ufanisi wa viuatilifu vya asili kabla ya kusajiliwa na kuruhusiwa kutumika, hatua inayolenga kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo zenye viwango vinavyokidhi matakwa ya kitaifa.
Naye mkulima mtafiti Julina David amesema pamoja na mafanikio yaliyopo, bado upatikanaji wa pembejeo za asili, hususan viuatilifu, ni changamoto kwa wakulima wengi kutokana na bidhaa hizo kutopatikana kwa urahisi katika maduka ya pembejeo.
Amesema pia ruzuku nyingi bado zinaelekezwa kwenye pembejeo za viwandani, hali inayopunguza kasi ya wakulima wengi kuhamia katika matumizi ya teknolojia za kilimo ikolojia hai.
“Tunahitaji kuimarisha elimu kuanzia ngazi ya kaya ili wananchi wajifunze kutengeneza mbolea na viuatilifu vya asili kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yao. Elimu ndiyo msingi wa mafanikio ya kilimo ikolojia hai,” amesema.
Naye mdau wa kilimo Ismail Shaban amesema kuna haja ya kuongeza uelewa wa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu vya asili ili kuongeza matumizi yake na kufanikisha malengo ya uzalishaji endelevu





