Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo, ametembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma kuangalia maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Matibabu, Mafunzo na Tafiti za Saratani hatua inayolenga kuimarisha huduma za kibingwa nchini.
Katika ziara hiyo Dkt. Msemo alipata fursa ya kujionea hatua iliyofikiwa ya mradi huo na kufanya mazungumzo ya kimkakati na Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi yaliyolenga kuendeleza ushirikiano baina ya taasisi hizo katika kuboresha huduma za saratani.
Akizungumza mara baada ya kuangalia ujenzi huo Dkt. Msemo alieleza kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa kituo hicho na kusisitiza kuwa ORCI iko tayari kushirikiana kwa karibu na BMH ili kuhakikisha kituo hicho kinaanza kutoa huduma za kibingwa, mafunzo kwa wataalamu pamoja na tafiti za kisayansi mara tu kitakapokamilika.
Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta ya afya huku akieleza kuwa ujenzi wa kituo hicho ni hatua muhimu katika kupanua huduma za saratani na kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaotegemea ORCI.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi aliwataka wakandarasi wa mradi huo Kampuni ya Mohamed Builders pamoja na Mshauri Elekezi wa mradi, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha wanakamilisha ujenzi kwa wakati uliopangwa ili wananchi waanze kunufaika na huduma hizo muhimu.
Mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 71 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2026 ukiwa na thamani ya Shilingi bilioni 32.








