Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, wameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya kuiendeleza Tanga kuwa kitovu cha nishati cha kikanda.
Hati hiyo ya Makubaliano imesainiwa leo, tarehe 6 Agosti 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa Ziara ya Kikazi ya Rais Museveni nchini kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Rais Dkt. Samia.
Makubaliano hayo yanahusisha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na Kampuni ya Biashara ya Mafuta na Nishati ya Vitol Bahrain E.C.
Awali, Rais Dkt. Samia alimkaribisha Rais Museveni Ikulu, ambapo viongozi hao walifanya mazungumzo ya ana kwa ana.
Akizungumzia makubaliano hayo, Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, alisema yanalenga kuiendeleza Tanga kuwa kitovu cha nishati cha kikanda kwa kutumia nafasi yake ya kimkakati ya kijiografia na miundombinu iliyopo ya usafirishaji wa nishati.
Alisema utekelezaji wa makubaliano hayo utaimarisha ushirikiano wa kikanda na kiuchumi, kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya nishati na kuongeza mchango wa Afrika Mashariki katika biashara ya nishati.
Waziri Ndejembi aliongeza kuwa makubaliano hayo yanaakisi dhamira ya nchi za Afrika kushirikiana kama washirika wa kimkakati katika kupanga, kufadhili na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kikanda.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Monica Masanza, alisema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kutekeleza maono ya muda mrefu ya ushirikiano wa Tanzania na Uganda katika sekta ya nishati.
Alisema sekta za nishati, mafuta na madini zina nafasi muhimu katika maendeleo ya Afrika, huku akieleza kuwa mradi huo utachochea ajira kwa vijana, kukuza biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Tanga pia ni kituo cha mwisho cha Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), linalojengwa kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga. Bomba hilo la inchi 24 lina urefu wa kilomita 1,443 na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 ya mafuta ghafi kwa siku kuelekea masoko ya kimataifa.







