Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ameipongeza JET kwa kazi kubwa inayofanya ya kuandika kuhusu uharibifu na utunzaji wa mazingira akibainisha kwamba JET ina jukumu muhimu la kuelimisha jamii na kulinda rasilimali zetu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ameishauri JET kuendelea na kazi nzuri inayofanya kuandika habari za kuelimisha kuhusu utunzaji wa vyanzo vya mito ili kulinda rasilimali za maji, kuzuia uharibifu wa mazingira, na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu athari za ukame na uchafuzi.
Msando ameyasema hayo jana tarehe, 6 Agosti 2026 wakati akifungua Jukwaa la Mkutano wa Taasisi Zisizo za Kiserikali (NGO’s) Wilaya ya Ubungo, ikibeba kaulimbiu isemayo “Fikra Mpya kuhusu Uendeshaji wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kupitia Vyanzo vya Ndani.”
Amezitaka Taasisi Zisizo za Kiserikali (NGO’s) zinazofanya kazi wilayani humo kuongeza ubunifu, kuimarisha ushirikiano na kutumia vyanzo vya ndani vya rasilimali ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utatuzi wa changamoto zinazoikabili jamii.
Katika mkutano huo, washiriki wamepokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mashirika kwa mwaka 2025, ikiwa ni pamoja na mafanikio, changamoto na mipango ya utekelezaji kwa kipindi kijacho. Mashirika yanayotekeleza shughuli katika sekta za Afya, Elimu, Mazingira, Uwezeshaji wa kiuchumi na kupambana na Ukatili wa kijinsia yamehimizwa kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika jamii ili kutoa suluhisho endelevu kwa changamoto zinazowakabili wananchi.
Msando pia amezitaka NGO’s ambazo bado hazijakamilisha taratibu za usajili na kupata vibali kuhakikisha zinazingatia sheria na kukamilisha taratibu hizo kwa wakati. Aidha, amekihimiza Chama cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania (NACONGO) kutumia ofisi za kata kama vituo vya kuratibu shughuli zake ili kuongeza ukaribu na jamii.
Vilevile, amewahimiza taasisi hizio kuwa wabunifu katika kubuni miradi na fursa za kiuchumi zitakazowawezesha kujitegemea kifedha na kufikia malengo ya maendeleo ya mashirika yao bila kutegemea wafadhili wa nje pekee.
Mkurugenzi wa JET John Chikomo alieleza kuwa JET imeona Umuhimu wa kuandika kuhusu vyanzo vya mito iliyopo katika Wilaya ya Ubungo na kwingineko ili:-
Kuongeza uelewa: Jamii inajifunza athari za shughuli za binadamu karibu na mito.
Kuhamasisha utunzaji: Kuelimisha watu kupanda miti na kuacha kilimo pembezoni mwa vyanzo vya maji.
Kuzuia uharibifu: Kutoa taarifa za haraka kwa mamlaka dhidi ya uharibifu wa mazingira.
Maeneo ya Kuzingatia Kwenye Habari
Shughuli za binadamu: kueleza athari za ufugaji na ukataji miti hovyo.
Sheria za mazingira: Kuelimisha umma kuhusu sheria zinazokataza kufanya shughuli karibu na vyanzo vya maji.
Suluhisho: Kuonyesha mbinu bora za kilimo na uhifadhi zinazofaa kutumika.




