Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) imeendesha mafunzo kuhusu nishati safi pamoja na kuileza kwa kina fursa ya mkopo nafuu wa ujenzi na uendeshaji wa vituo vidogo vya mafuta ya petroli na dizeli vijijini kwa Viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) pamoja na Viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika wapatao 300 katika jengo la kijiji cha ushirika katika viwanja vya maonesho ya Nane Nane vya John Malecela, Nzuguni Jijini Dodoma.
Akiendesha mafunzo hayo kutoka REA; Mhandisi, Deusdedit Malulu amewaeleza Wanaushirika hao kuwa Wakala (REA) imeanza rasmi utoaji wa mikopo nafuu ya ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijini na kwamba Mradi huo unalenga kuondoa hatari za moto na ajali zinazotokana na uuzaji au uhifadhi wa mafuta kwenye chupa za plastiki na magaloni yasiyokidhi viwango vya usalama.
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ushirikiano na Benki ya Azania ilizindua rasmi mradi huo mkubwa tarehe 23 Julai, 2026; Mradi wa utoaji wa mikopo nafuu kwa wajasiriamali wadogo, utakaofanikisha ujenzi na uendeshaji wa vituo vidogo vya kuuza mafuta ya petroli na dizeli maeneo ya vijijini.
“Wananchi wengi wa vijijini wamekuwa wakinunua mafuta kwa gharama kubwa na wakati mwingine kutoka kwa wauzaji wasio rasmi, jambo linaoongeza hatari za kiusalama, ubora hafifu wa mafuta pamoja na kupanda kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji,”amesema Mhandisi Malulu.
Mhandisi Malulu aliongeza kuwa licha ya fursa hiyo ya mkopo yenye masharti nafuu, REA pia imekuwa ikitoa fursa za miradi ya nishati safi za kupikia pamoja na miradi ya nishati jadidifu; ikiwemo utoaji wa ruzuku na mikopo yenye masharti nafuu kwa miradi ya nishati za kuzalisha umeme unaotokana na vyanzo vya maji; upepo pamoja jua.









