Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilimanjaro
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kwa kushirikiana na mkandarasi wake EITS, umefadhili vijana 17 wa Kitanzania kusomea mafunzo ya Ufundi Stadi Ngazi ya III katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendeleza ujuzi na kuongeza ajira kwa vijana.
Vijana hao watapata mafunzo katika fani mbalimbali zinazohitajika katika soko la ajira, ikiwemo muziki na ala zake, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ufundi wa simu za mkononi pamoja na uendeshaji wa mitambo mbalimbali ya viwandani.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha wadau wa programu hiyo mjini Moshi, Mkuu wa Maudhui ya Ndani na Uwezeshaji wa EACOP, Bi. Martha Makoi aliishukuru VETA Moshi kwa ushirikiano wake katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo na kutoa mafunzo yenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya sekta ya viwanda.
Alisema kuwa baada ya kutangazwa kwa fursa hizo, EACOP ilipokea jumla ya maombi 78 kutoka vijana wa maeneo mbalimbali nchini waliokidhi masharti ya awali, ambapo baada ya mchakato wa usaili na tathmini, wanafunzi 17 walichaguliwa kufadhiliwa.
“Programu hii ni sehemu ya dhamira pana ya EACOP ya kuendeleza ujuzi na kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata uwezo wa kuajiriwa katika miradi mbalimbali ya kitaifa na kimataifa na mamia ya vijana wamefaidika kupitia vyuo mbalimbali hapa nchini,” alisema Bi. Makai.
Aliongeza kuwa uwekezaji katika elimu ya ufundi utasaidia kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi nchini, kuimarisha ushindani wa nguvu kazi ya Tanzania na kuchochea maendeleo ya sekta ya viwanda nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo wa EITS, Bw. Sweetbert Mahemba, alisema programu hiyo inaonyesha dhamira ya kampuni hiyo katika kukuza ushiriki wa Watanzania katika miradi mikubwa kupitia maendeleo ya rasilimali watu wenye ujuzi.
“EITS inajivunia kushirikiana na VETA Moshi kuwapatia vijana ujuzi wa vitendo unaohitajika katika sekta ya viwanda ili kuongeza fursa za ajira na kuchangia maendeleo ya viwanda nchini,” alisema Bw. Mahemba.
Aliongeza kuwa mpango huo wa ufadhili ni sehemu ya mkakati mpana wa EACOP wa kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya miundombinu inaacha urithi wa maendeleo ya kijamii unaodumu hata baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bomba hilo.
Naye Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kaskazini, Bi. Monica Mbelle, alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya ufundi stadi kama njia ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kupata ajira zenye tija.
“Mafunzo haya ya Ngazi ya III yatawapatia washiriki ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, kuongeza fursa za ajira na kujiajiri, pamoja na kufungua njia za maendeleo ya taaluma zao,” alisema Bi. Mbelle.
Akizungumza kwa niaba ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Bw. Stephen Mjema aliwapongeza wanafunzi waliopata ufadhili huo na kuwahimiza kutumia vyema nafasi waliyopewa kwa kuwa na nidhamu, kujituma katika masomo na kuwa mabalozi wazuri wa programu hiyo.
Kwa mujibu wa EACOP, mradi huo tayari umetoa ufadhili wa masomo kwa zaidi ya wanafunzi 300 katika taaluma mbalimbali za ufundi na teknolojia, hatua inayodhihirisha dhamira yake ya kuacha urithi wa maendeleo endelevu kupitia uwekezaji katika rasilimali watu.
Mradi wa EACOP unamilikiwa na TotalEnergies yenye hisa asilimia 62, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) kila moja ikimiliki asilimia 15, na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya China (CNOOC) ikimiliki asilimia nane.
Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) lina urefu wa kilometa 1,443, likianzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, mkoani Tanga nchini Tanzania. Ndani ya Tanzania, bomba hilo linapita katika mikoa minane ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

