Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Madereva wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani wametakiwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani na kuacha kutumia nafasi zao kama askari kukiuka sheria wanapokuwa barabarani.
Rai hiyo imetolewa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Edson Mwakihaba, wakati akitoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva 26 wa magari ya Jeshi la Polisi mkoani humo, katika Ukumbi wa Benjamin Mkapa.
Mwakihaba alisema madereva hao wanapaswa kuwa mfano kwa jamii kwa kuzingatia mwendokasi unaotakiwa, kuepuka kuendesha wakiwa walevi, kufanya overtaking kwa usalama, pamoja na kuheshimu vivuko vya watembea kwa miguu na taa za barabarani.
Alieleza matumizi ya nafasi au mamlaka ya kipolisi si sababu ya dereva kuvunja sheria za barabarani, akisisitiza kuwa makosa yanayofanywa na madereva yanaweza kuwa chanzo cha ajali na kusababisha madhara kwa watu na mali.
Aidha, Mwakihaba aliwataka madereva hao kuzingatia taratibu za matumizi ya magari ya Polisi, ikiwemo matumizi sahihi ya logbook, Force Order na maelekezo yanayohusu hatua za kuchukua endapo gari la Polisi litapata ajali.
Alisema mafunzo ya udereva yanapaswa kuendelea kutolewa ili kuongeza ufanisi wa madereva, kupunguza ajali na gharama za matengenezo ya magari ya Serikali.
Katika mafunzo hayo, madereva hao pia wamehimizwa kujiendeleza kwa kusoma ili kuendana na mabadiliko ya magari ya kisasa yanayotumiwa na Jeshi la Polisi, pamoja na kuwa na nidhamu, uadilifu na uzalendo wakati wote wanapokuwa kazini.






