Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wanaohudhuria mafunzo maalum ya diplomasia nchini India wametembelea Ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini New Delhi.

Katika ziara hiyo, watumishi hao walikutana na wafanyakazi wa Ubalozi na kupata fursa ya kuzungumza na Balozi wa Tanzania nchini India, Mheshimiwa Anisa Mbega, pamoja na watumishi wengine wa Ubalozi.

Akizungumza wakati wa kuwakaribisha watumishi hao Ubalozini, Mheshimiwa Balozi Anisa Mbega alisema Ubalozi umefurahi kuwapokea watumishi wenzao kutoka Wizara na kuwapongeza kwa kupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo maalum ya diplomasia.

Balozi Mbega alisema ana imani kuwa mafunzo waliyoyapata yamewaongezea maarifa na hivyo yatachangia kuboresha utendaji wao wa kazi na hivyo kuleta tija na ufanisi kwa Wizara.

Aliishukuru Serikali ya India kwa kuitikia ombi la Wizara la kuwajengea watumishi uwezo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa tija na ufanisi na kuongeza kuwa Ubalozi utaendelea kushirikiana na Serikali ya India ili kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na India

Watumishi hao wa Wizara walikuwa nchini India kwa mafunzo maalum ya muda mfupi yaliyofadhiliwa na Serikali ya India na kutolewa na Chuo cha Sushma Swaraj (Sushma Swaraj Institute of Foreign Service – SSIFS), yakilenga kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara katika maeneo ya diplomasia ya kisasa, masuala ya kimataifa na kikanda, historia, mabadiliko ya kidigitali,utamaduni na sera ya mambo ya nje ya India.