Na Mwandishi Wetu , JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wazalishaji wa nishati mbadala ya kupikia, hususan mkaa unaotokana na taka ngumu, wametakiwa kuendelea kutumia teknolojia na mbinu za kisayansi katika uzalishaji ili kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi ubora na viwango vinavyokubalika, hatua itakayowawezesha kupata masoko ya ndani na ya kimataifa.

Ushauri huo umetolewa leo, Agosti 17, 2026, jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Shirika la Utafiti kuhusu Kupunguza Umaskini REPOA, Dkt. Jamal Msami, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa wadau wanaozalisha nishati mbadala ya kupikia kwa kutumia taka ngumu.

Dkt. Msami amewapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa kutambua kuwa nishati mbadala ni eneo lenye fursa kubwa za kibiashara, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sayansi katika uzalishaji ili bidhaa zinazotengenezwa ziwe na tija na ziweze kushindana sokoni.

“Niwapongeze kwa kutambua kuwa ili biashara ifanyike kwa tija na kuleta faida, ni lazima utangulize sayansi mbele. TIRDO inawapatia mafunzo yanayokwenda kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye ubora zaidi,” amesema Dkt. Msami.

Amesema mafunzo hayo yanahusisha mada mbalimbali zitakazowasaidia wazalishaji kuboresha bidhaa zao kwa kuzingatia afya na usalama wa watumiaji, ili kuhakikisha nishati hiyo inakuwa salama na yenye manufaa kwa wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania TIRDO, Humphrey Ndossi, amesema shirika hilo linaendelea kuwaongezea ujuzi wazalishaji wa nishati mbadala kwa lengo la kuongeza thamani ya bidhaa zao na kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyohitajika katika masoko ya ndani na ya kimataifa.

Ndossi amesema kumekuwa na malalamiko kuhusu ubora wa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa, hivyo amewataka wazalishaji kutumia maarifa wanayopata kupitia mafunzo hayo kuboresha uzalishaji wao na kuzingatia viwango vinavyowekwa.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka Tanga, Omary Ahmadi, ameshukuru TIRDO kwa kuwawezesha kupata mafunzo hayo, akisema yatawasaidia kuboresha uzalishaji wa nishati mbadala na kutengeneza bidhaa bora na salama kwa matumizi ya wananchi.

Amesema awali baadhi yao walikuwa wakizalisha bidhaa bila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu viwango vya ubora na usalama wa afya, huku matumizi ya nishati mbadala yakisaidia pia kupunguza utegemezi wa kuni na hivyo kuchangia katika uhifadhi wa misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.