Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,
Dar es Salaam
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umesaini Mkataba wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) na Kampuni ya Galco Limited kwa ajili ya kuendeleza eneo la Kiwanja Na. 264, Temeke Mwisho jijini Dar es Salaam, kupitia ujenzi wa mradi wa “Modern Logistics Hub.”
Mradi huo unalenga kuongeza ufanisi katika huduma za usafirishaji na upokeaji wa mizigo, pamoja na kutoa suluhisho la changamoto ya maegesho ya malori na kupunguza mlundikano wa malori katika maeneo ya jiji.
Akizungumza Agosti 18,2026 Jijini Dar es salaam mara baada ya hafla ya kusaini mkataba huo, Mkuu wa Kitengo cha PPP, Marko Silali, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendeleza na kuongeza thamani ya mali za TBA.
Silali amesema mradi huo unatarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira, kuboresha mandhari ya jiji na kupunguza utegemezi wa Serikali katika kugharamia shughuli za maendeleo.
“Tunamshukuru mwekezaji huyu kwani tunaamini mradi huu utasaidia kutatua changamoto ya mlundikano wa malori, kuleta chachu ya uchumi, ajira na kuboresha mandhari, pamoja na kupunguza utegemezi wa Serikali,” amesema Silali.
Kwa upande wake, Meneja wa Miradi ya Kimkakati wa Galco Limited, David I. Kapesa, amesema kampuni hiyo imeona fursa ya uwekezaji kutokana na mipango ya Serikali ya kupanua Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza uwezo wa usafirishaji kupitia reli.
Kapesa amesema Galco Limited, ambayo inajihusisha na huduma za usafirishaji na upokeaji wa mizigo bandarini inayopita nchini pamoja na mizigo inayobakia nchini, imeamua kutumia fursa hiyo kuwekeza katika ujenzi wa kituo hicho cha kisasa cha usafirishaji.
Amesema mradi huo ni sehemu ya mwendelezo wa ushirikiano mzuri kati ya kampuni hiyo na taasisi za Serikali katika kuchochea shughuli za kiuchumi, huku akiahidi kuwa Galco Limited itajenga kituo bora kitakachokuwa na mchango mkubwa katika kuongeza fursa za kiuchumi katika eneo la Temeke.
Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji na uhifadhi wa mizigo, kupunguza msongamano wa malori barabarani na kuchochea ukuaji wa biashara zinazohusiana na sekta ya usafirishaji na lojistiki nchini.






