Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua za El Nino zitakazoathiri msimu wa mvua za Vuli unaotarajiwa kuanza mapema Oktoba 2026 na kuendelea hadi Januari 2027.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Agosti 18, 2026 Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema msimu wa mvua za Vuli 2026 unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Nino yenye nguvu kubwa, huku mvua za juu ya wastani hadi wastani zikitarajiwa katika maeneo mengi.
Amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Septemba hadi wiki ya kwanza ya Oktoba 2026 katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria na baadaye kusambaa katika maeneo mengine mwezi Oktoba.
Amesema mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika Kanda ya Ziwa Victoria, ikijumuisha Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara, pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Aidha, mvua hizo zinatarajiwa katika Dar es Salaam, Tanga, Pwani ikiwemo Mafia, kaskazini mwa Morogoro, Unguja na Pemba, pamoja na Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Dkt. Chang’a amesema kwa kawaida mvua za Vuli huisha mwezi Desemba, lakini katika msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea hadi Januari 2027, huku ongezeko la mvua likitarajiwa katika mwezi Novemba 2026.
Amesema vipindi vya unyevu kupita kiasi kwenye udongo pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, huku magonjwa ya mazao yanayosababishwa na kuvu, bakteria na virusi yakitarajiwa kujitokeza.
“Mvua za muda mrefu zinaweza kuathiri shughuli za uvunaji na kusababisha upotevu wa mazao baada ya kuvuna. Hata hivyo, shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama ilivyo kawaida katika baadhi ya maeneo katika msimu huu wa Vuli, 2026,” amesema.
Aidha, amesema ongezeko la kina cha maji katika mabwawa na mito linatarajiwa kujitokeza, hali ambayo inaweza kuathiri miundombinu ya rasilimali za maji na nishati, huku magonjwa ya mlipuko yakitokea kutokana na uchafuzi wa maji.
Dkt. Chang’a amewataka wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati, pamoja na kutumia mbinu bora za kuzuia maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba.
Ametoa tahadhari pia kwa wadau wa usafirishaji, akisema hali mbaya ya hewa inaweza kuathiri miundombinu na shughuli za usafirishaji kwa njia za barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege, ikiwemo mmomonyoko wa udongo, kuporomoka kwa kingo za barabara, uharibifu wa madaraja na njia za reli za MGR na SGR.
Aidha, amesisitiza wito wa tahadhari kwa wadau wa mifugo na uvuvi, utalii na wanyamapori, nishati na madini, sekta ya afya, Serikali za Mitaa, ujenzi, sekta binafsi pamoja na Menejimenti za Maafa za wilaya, mikoa na kitaifa ili kuendelea kuratibu mipango ya kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.




