Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kupitia Mwenyekiti wake Mhe.Deodatus Mwanyika, ameipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zake kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake ya udhibiti ubora kwa ufanisi .

Mhe. Mwanyika amesema kuwa juhudi zinazofanywa na TBS katika kuhakikisha usalama na ubora wa bidhaa zinazotumiwa na Watanzania zinaonekana,  sambamba na kuendelea kutoa Elimu na kuongeza programu maalum za kushughulikia bidhaa zinazoingizwa nchini kwa njia zisizo rasmi.

Aidha, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imepongezwa kwa maboresho na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake na kusisitizwa kuongeza kasi ya utoaji Elimu kuhusu mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS) ili wakulima na wadau wengi zaidi wanufaike.

Kwa upande wake Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb) amesema Wizara hiyo imepokea pongezi hizo pamoja na  maelekezo na ushauri uliotolewa na Kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha huduma na kuongeza ufanisi katika sekta ya viwanda na biashara nchini.