*Akemea viongozi wasiokuwa na msimamo ndani ya Chama
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia haki kwa kutoegemea maslahi binafsi huku akikemea viongozi wasiokuwa na msimamo ndani ya CCM.
Wasira aliyasema hayo alipozungumza na viongozi pamoja na wanachama wa CCM wilayani Iramba mkoani Singida, leo (Agosti 20, 2026) ambapo aliwataka wanachama kufuata misingi inayozingatia haki katika uchaguzi wa viongozi ndani ya CCM.
“CCM inahitaji viongozi wenye msimamo katika mambo ya msingi na wasiobadilika kutokana na mazingira au maslahi binafsi. Tunataka uongozi ambao hayumbi. Tunataka mtu ambaye ana msimamo kwa mambo ya msingi. Huyo ndiye kiongozi wetu,” amesisitiza.
Alitoa wito kwa wanachama wa CCM kuhakikisha wanachagua viongozi kwa kuzingatia uwezo, uadilifu na misingi ya haki huku akionya dhidi ya viongozi wanaopatikana kwa rushwa.
Alisema CCM haipaswi kuruhusu uongozi unaotokana na rushwa, vitisho au ujanja wa aina yoyote kwa kuwa viongozi wanaochaguliwa ni kielelezo cha Chama katika jamii.
“Wanachama ndiyo wenye jukumu la kuhakikisha watu wanaopewa dhamana ya kuongoza Chama wana sifa na uwezo unaohitajika. Sisi ndiyo tunateua wanachama. Msije mkakubali Chama chetu kikapata uongozi unaotokana na rushwa bila uwezo wa kuongoza,” alisema.
Alieleza kuwa viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali wana majukumu ya kuwateua au kusimamia mchakato wa kupata viongozi wa chini yao, hivyo wanapaswa kuwa waangalifu katika maamuzi wanayofanya.
Wasira alisema wenyeviti wa wilaya wanahusika na uteuzi wa viongozi wa matawi, huku wenyeviti wa mikoa wakiwa na jukumu katika uteuzi wa viongozi ngazi ya kata.
Ameonya kiongozi atakayebainika kutumia nafasi yake vibaya kwa kupokea rushwa na kuteua viongozi wasio na uwezo, hatakiwi kuachwa bila kuwajibishwa.
Wasira amesisitiza kuwa viongozi wote wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu na misingi ya Chama.
Amesema mfumo huo wa uwajibikaji unatakiwa kuanzia ngazi za chini hadi Halmashauri Kuu ya CCM, ili kuhakikisha viongozi wanatimiza wajibu wao ipasavyo.
Amesema kiongozi hawezi kutumia utajiri wake kama kipimo cha uwezo wa kuongoza, akisisitiza kuwa fedha haziwezi kuongeza uwezo wa mtu katika uongozi.
Vilevile, Wasira amesema kila kiongozi anapaswa kujipima na kutathmini kama bado ana uwezo wa kuongoza kulingana na mahitaji ya wakati husika.
Amesema uwezo wa kuongoza siyo jambo la kudumu kwa mtu katika maisha yake yote, hivyo kiongozi anapaswa kuwa tayari kumpisha mwingine pale anapoona hana tena uwezo unaolingana na mahitaji ya wakati.
“Huwezi ukasema uwezo wangu umeshuka lakini hela yangu imeongezeka, kwa hiyo hela itaongeza uwezo?. Hakuna. Hela haiongezi uwezo wa kuongoza,” amesisitiza.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuwa na viongozi wenye uwezo wa kukemea na kujibu upinzani kwa hoja, badala ya kutumia vitisho au mbinu zisizo za haki.
Amesema viongozi wa CCM wanapaswa kuchaguliwa kwa hiyari ya wapiga kura, bila rushwa, vitisho wala ujanja wa aina yoyote.
Kwa mujibu wa Wasira, kiongozi anayechaguliwa kwa misingi hiyo anakuwa kielelezo cha Chama kwa wananchi kwa kuwa jamii humtazama kiongozi huyo kama sura ya CCM.
Amesema endapo kiongozi atakuwa mwadilifu, mwenye uwezo na anayezingatia misingi ya Chama, wananchi wataona taswira nzuri ya CCM.
Wasira ametoa wito kwa wanachama wa Iramba na Mkalama kutumia nafasi yao kwa busara katika uchaguzi wa viongozi, akisisitiza kuwa lengo ni kujenga Chama chenye viongozi wenye uwezo, uadilifu na msimamo.
“Ndiyo maana tunawaambia tunataka tubadilike, tutoke kwenye uchepuko, twende njia kuu. Njia kuu inatutuma tutumie misingi ya haki katika kuchagua viongozi wetu,” alisema.






