WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuendelea kuliombea Taifa na kudumisha amani, akisema amani ni msingi unaowezesha wananchi, taasisi za dini na Taifa kwa ujumla kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.
Amesema dunia inaendelea kushuhudia mabadiliko na mitikisiko katika maeneo mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kumwomba Mungu ailinde Tanzania na kuendeleza amani ambayo imeiwezesha nchi kutekeleza shughuli zake kwa utulivu.
Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumapili, Agosti 23, 2026) aliposhiriki ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Usharika wa Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
“Tuendelee kuiombea nchi yetu. Leo hii tunaweza kufanya ibada kwa sababu nchi yetu ipo na amani. Tuna mipango mbalimbali kama nchi, katika ngazi ya familia, taasisi, Dayosisi na Kanisa, lakini hayo yote tunaweza kuyafanya kama nchi yetu ipo na amani,” amesema.
Dkt. Mwigulu amewafikishia waumini salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali kwa ujumla, huku akitambua na kuenzi mchango mkubwa unaofanywa na Kanisa katika maendeleo ya nchi.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kusonga mbele.
“Hauwezi ukataja maendeleo ya nchi yetu bila kutaja mchango wa Kanisa,” amesema.
Naye Katibu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Bw. Goodluck Nkini, alimshukuru Waziri Mkuu kwa kuchagua kuabudu katika Usharika wa Kijitonyama na kwa kuendelea kujumuika na waumini katika maeneo mbalimbali.
Ibada hiyo iliongozwa na Mchungaji Anna Kuyonga wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Kijitonyama.
Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mhe. Aggrey Mwanri; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila; Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule; Mbunge wa Same Magharibi, Dkt. David Mathayo; na Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga









