Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia Mirerani
WAZIRI wa Madini Anthony Peter Mavunde ameingilia kati changamoto ya bei kubwa ya ankara ya matumizi ya nishati ya umeme kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani Wilayani wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Mavunde akizungumza katika ziara machimbo ya madini ya Tanzanite ameagiza wadau wa madini kukutana na Mkurugenzi mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange.
Amesema wadau wa madini ya Tanzanite wakiongozwa na kamishna wa madini Dk Abdulrahaman Mwanga wakutane na Twange na uongozi wa TANESCO jijini Dodoma Agosti 27, 2026.
“Hili suala la bei kubwa ya ankara ya umeme wanayoletewa wachimbaji madini ni dogo mno na litamalizwa na Mkurugenzi mtendaji wa TANESCO hata Waziri wa Nishati halitamfikia,” amesema Waziri Mavunde
Ametoa agizo hilo baada ya kusikiliza kilio cha bei kubwa ya ankara ya matumizi ya nishati ya umeme kwa wachimbaji hao wa madini ya Tanzanite.
Awali, Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi amesema ankara kubwa wanayopewa wachimbaji na TANESCO imekuwa kero kubwa kwao.
“Wachimbaji madini wa Mirerani wanaletewa ankara kubwa ya umeme utadhani wana viwanda kwa kuwekwa kwenye matumizi makubwa ya KVA, hivyo wanaomba waondolewe hapo wawe wanalipia kawaida,” amesema Elisha.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya ambaye pia ni mbunge wa Simanjiro amepongeza hatua hiyo ya Waziri Mavunde kuingilia kati kero ya umeme.
“Wachimbaji wamefarijika mno baada ya wewe Waziri kutoa maelekezo ya wadau wa madini ya Tanzanite kwenda Dodoma kukutana na Tanesco kumaliza kero hiyo,” amesema Ole Millya..

Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining & Gem LTD wanaochimba kitalu C kwa ubia na serikali, Onesmo Mbise amesema wao huwa wanalipia umeme Sh100 milioni kwa mwezi mmoja.
Mbise amesema wachimbaji wamewekwa kwenye mfumo unaowabana kulipa bei kubwa ya nishati ya umeme katika machimbo hayo ya madini ya Tanzanite.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro, Warda Abeid Maulid amesema wameyapokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mavunde hivyo watayatekeleza.
“Kwa niaba ya viongozi wa wilaya na mkoa tunakukaribisha tena eneo hili la mji mdogo wa Mirerani katika kuhakikisha tinapambana kuondoa changamoto zilizopo,” amesema Warda.



