Na Byarugaba Innocent OR-MV

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe.Joel Arthur Nanauka Agosti,2026 ameendelea kuchanja mbuga kuwafikia Vijana wa Kitanzania safari hii akitia nanga katika Kijiji cha Makunda,Mkoani Singida ambapo amewakabidhi Mitambo mitatu yenye thamani ya Milioni 263 kurahisisha uchakataji malighafi Kiwanda cha Makunda zinazotokana na programu ya uwezeshaji Vijana kiuchumi kupitia Bilioni 200.

Mkurugenzi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi Edward Simon Haule akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Vijana Bi.Jenifa Christian Omolo amesema Serikali itaendelea kuwafikia Vijana kupitia Viwanda vidogo vidogo vinavyolenga kuongeza tija ya uzalishaji,kuongeza mnyororo wa thamani kwa bidhaa zinazozalishwa na kupanua wigo wa ajira kwa Vijana wengine

Haule amebainisha kuwa shilingi Milioni 263 zimenunua mashine tatu Mpya ambazo ni kinu cha kukamua Alizeti na Filta kwa Milioni 18.9,Mashine Mpya ya kukamua na kuchuja mafuta kwa Milioni 26,Gari Mpya aina ya Howo 4×2 Make SINOTRUCK kwa Milioni 97.63 huku fedha nyingine ikitolewa kwa ajili ya kununua vifungashio.

Msimamizi Kiongozi wa Kiwanda hicho Orgenesi Andrew Yindi amesema kilio cha muda mrefu cha kukosa ya Mitambo na gari kubwa la kukusanyia malighafi na kusambazia bidhaa limepata muarobaini kutoka kwa Serikali ya awamu sita inayoongozwa na Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Programu ya uwezeshaji Vijana kiuchumi hali inayokwenda kutimiza ndoto za Vijana na Wakulima wa Vijiji vilivyopo Kata ya Kyengege Wilaya ya Iramba.

Yindi amesema kuwa Mitambo hiyo inakwenda kuongeza ajira kwa Vijana kutoka 10 waliopo sasa mpaka 60 huku uzalishaji ukipanda kufikia tani 11 kutoka tani 2.5 zinazozalishwa sasa.
“Mashine hizi zina uwezo wa kuchakata kilo 6500 za Alizeti kwa siku sawa na kilo 45,500 kwa wiki ambapo kwa Mwezi Kiwanda kinaweza kuchakata kilo 182,000” amesema Yindi

Akizungumzia Gari,Yindi amesema kuwa litawasaidia kusafirisha bidhaa zinazozalishwa kiwandani mathalan mafuta kutoka dumu 18 zilizo kuwa zikisafirishwa awali kwa Krikuu mpaka dumu 400 sambamba na kulitumia kukukusanyia wastani wa magunia 600 ya Alizeti kwa siku.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Vijana Happyness Mgwando amewapongeza Vijana wa Makunda kwa kuendelea kujishughulisha hata kabla ya kuweseshwa na Serikali na kutoa rai kwa Vijana wengine nchini kuiga mfano huo huku akitoa rai ya kujiepusha na tamaa ili kufikia Malengo.