Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (TASAC) imesimamisha utoaji wa
leseni mpya za Bandari Kavu za Makontena (ICD) kufuatia kuongezeka kwa malalamiko ya wananchi kuhusu vituo hivyo vinavyoanzishwa katika
maeneo ya mijini na kusababisha ongezeko la malori na foleni mitaani.
Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, amesema uamuzi huo umefikiwa
baada ya mamlaka hiyo kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi
pamoja na maombi mengi ya watu waliokuwa wakitaka kuanzisha ICD mpya.
Amesema TASAC imeamua kusimamisha utoaji wa leseni hizo kwa muda na
kutoa notisi kwa umma kwamba hakuna mtu anayepaswa kuendeleza eneo la
ICD bila kupata kibali cha TASAC.
Salum amesema TASAC inafanya tathmini ya uwezo wa ICD zilizopo
kuhudumia shehena zinazopita katika Bandari ya Dar es Salaam, na
inatarajia kufanya tathmini nyingine mwezi Oktoba ili kubaini mahitaji
halisi ya maeneo hayo.

Hatua hiyo imekuja wakati kukiwa na mjadala kuhusu kuongezeka kwa
bandari kavu katika maeneo ya mijini.
Salum amesema kabla ya mwaka 2000 shughuli nyingi za kuhifadhi na
kuhudumia shehena zilifanyika ndani ya Bandari ya Dar es Salaam lakini ongezeko la mizigo lilisababisha msongamano na kulazimisha mamlaka kutafuta maeneo ya nje ya bandari kwa ajili ya kuhifadhi na kushughulikia sehemu ya shehena.
Amesema Bandari ya Dar es Salaam, ambayo awali ilikuwa ikihudumia
takribani makontena 110,000, ilifikia takribani makontena 340,000 mwaka 2008,hali hiyo ilifanya ICD kuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa usafirishaji kwa kusaidia kuhifadhi makontena na kufanya baadhi ya kuhughuli za ukaguzi na forodha nje ya bandari.
‘’Kwa sasa,kuna idadi ya makontena imeendelea kuongezeka, kutoka
740,000 mwaka 2020 hadi 1,085,000 mwaka 2025, ongezeko la zaidi ya
asilimia 50.
Kutokana na ongezeko hilo, baadhi ya ICD zimekuwa zikikabiliwa na
mzigo mkubwa kuliko uwezo wao.katika kipindi cha mwaka jana hadi
Machi, baadhi ya vituo vilikuwa na uwezo wa kuhifadhi makontena 200
lakini vikapokea zaidi ya 300’’Amesema.
Salum amesema wamewataka waendeshaji wa ICD kuhakikisha malori
yanaingia na kuhifadhiwa ndani ya maeneo yao badala ya kusubiri katika
mitaa inayozunguka vituo hivyo. Salum alisema zaidi ya ICD sita zilisitishwa wiki iliyopita na kupewa maelekezo ya kuandaa maeneo ya kuhifadhi malori, huku ICD zote zikitakiwa kuongeza maeneo ya kuhifadhi makontena.
Amedai pamoja na Serikali kuendelea kuboresha usafiri wa reli, uwezo
wake bado hautoshi kubeba shehena yote inayopita bandarini, hivyo malori yanaendelea kuwa muhimu katika kusafirisha makontena kwenda ICD
mbalimbali.
Mkurugenzi wa Bandari, Abed Gallus, amesema ushirikishwaji wa sekta
binafsi umeongeza ufanisi wa bandari, huku kiasi cha mizigo kikiongezeka kutoka tani milioni 23.7 mwaka 2023/2024 hadi tani milioni 33.7 mwaka 2025/2026.
Mwaka 2025/2026 imehudumia makasha 1,300,000, hivyo kuwepo kwa makasha
zaidi ya uwezo wa Kwala kumeendelea kuhitaji kuongeza uhamishaji wa
mizigo kwa njia ya reli.
‘’Changamoto kubwa iliyokuwepo ilikuwa uwezo mdogo wa reli ya zamani,
uliosababisha idadi ya safari za treni kwenda Kwala kutokidhi mahitaji,baada ya kubaini TRC imejenga eneo la kupakia mizigo ya SGR litakalokuwa na uwezo wa kusafirisha hadi makasha 400 kwa siku,
ikilinganishwa na takribani makasha 20 kwa siku yanayosafirishwa kwa
sasa.

Kwa kutumia SGR, uwezo wa kusafirisha makasha kwenda Kwala unatarajiwa
kuongezeka mara kumi ya kiwango cha sasa, itatumika kusafirisha mizigo
kwenda Ihumwa, Morogoro, ambako inatarajiwa kuwepo kwa ongezeko kubwa
la shehena’’Amesema
Gallus amesema huduma za ICD zimechangia kupunguza muda wa meli kukaa nandarini, akitoa mfano wa makontena ambayo sasa yanaweza kuhudumiwa ndani ya siku chache ikilinganishwa na muda mrefu uliokuwa ukitumika hapo awali.
Mkurugenzi wa Uchukuzi TASAC, Nahson Sigalla, amesema ongezeko la
makasha lisipodhibitiwa linaweza kusababisha msongamano bandarini,
kuchelewesha meli na kuongeza gharama za usafirishaji kwa waagizaji wa
mizigo.
Mwenyekiti wa Waendesha Bandari Kavu Tanzania, Meleck Shang’e, amesema
ICD zina jukumu la kuongeza wigo wa Bandari ya Dar es Salaam kwa
kuhamisha baadhi ya shughuli nje ya bandari,ambapo baadhi ya shehena
vinaweza kuhifadhiwa nje ya bandari ili kupunguza msongamano na kuwezesha bandari kuhudumia meli kwa ufanisi zaidi.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ni Deodatus Balile
amesema wananchi wamekuwa wakilalamikia kuwepo kwa ICD katika maeneo ya makazi kutokana na malori mengi yanayoingia na kutoka katika vituo
hivyo na kusababisha foleni

