Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kwa mara ya kwanza watalamu wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na mwenzao kutoka Mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada lililopo nchini Uingereza Dkt. Ahmet Sasmazel wamemfanyia upasuaji wa moyo mtoto aliyezaliwa na mishipa miwili mikubwa ya damu inayotoka kwenye moyo kupishana (Nikaidoh Operation).

Upasuaji huo umefanyika kwa njia ya kufungua kifua kwa mtoto mwenye umri wa miaka miwili na mwezi mmoja kwa mafanikio makubwa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Thabit Ramadhani alisema upasuaji huu ni wa kwanza kufanyika JKCI na Afrika Mashariki na Kati.

“Tumefanya upasuaji huu kwa umakini mkubwa, na sasa mtoto anaendelea vizuri, ameshatolewa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) na kupelekwa katika chumba cha ungalizi wa watoto (PICU)”, alisema Dkt. Thabit.

Dkt Thabit alisema mtoto huyo mbali na kuwa na mishipa mikubwa ya damu inayotoka kwenye moyo kupishana pia alikuwa na tundu kwenye moyo pamoja na uvimbe uliosababisha mshipa wa damu kusinyaa hivyo kuzuia damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye mwili na mapafu kwa mtiririko unaostahili.

“Tatizo hili la mshipa wa damu unaopeleka damu kwenye mapafu kusinyaa ulisababishwa na kukandamizwa na uvimbe aliokuwa nao mtoto hivyo kutoruhusu damu kupita kwa urahisi, tumemuwekea mtoto mrija wa damu bandia ili kuwezesha damu kwenda kwenye mapafu”, alisema dkt. Thabit.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada lililopo nchini Uingereza Dkt. Ahmet Sasmazel alisema mafanikio ya upasuaji huo yametokana na ushirikiano wa karibu uliokuwa ukifanywa na watalaamu wa JKCI.

“Tumepata matokeo mazuri ya upasuaji huu kwasababu ya uwepo wa vifaa tiba vya kisasa na watalaamu waliobobea ambao wana moyo wakuhudumia watoto kama hao na kujikita katika kuokoa maisha yao, waendelee kujifunza kwaajili ya matokeo mazuri zaidi ya baadaye”, alisema Ahmet.

Naye mama wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji huo Witness Kibuga alisema mtoto wake aligundulika kuwa na tatizo la moyo akiwa na umri wa miezi saba na kuanza kuudhuria kliniki ya matibabu ya moyo hadi sasa alipofanyiwa upasuaji huo.

“Namshukuru Mungu na watalaamu wote wa JKCI kwa kumfanyia upasuaji mtoto wangu ambaye kwa sasa anaendelea vizuri naomba waendelee na moyo wa kuwahuduma watoto wetu na kuokoa maisha yao kwani tunawategemea sana”, alisema Witness.

Mama wa mtoto Deus Mgonzo, Witness Kibuga akiwa na Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Idd Kimaro katika chumba cha ungalizi wa watoto (PICU) alipolazwa mtoto huyo jijini Dar es Salaam.
Wataalamu wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimfanyia upasuaji wa moyo mtoto wa miaka miwili (Nikaidoh Operation) kwa kushirikiana na daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Uturuki Ahmet Sasmazel wa Mradi wa Liitle Aid wa Shirika la Muntada Aid jijini Dar es Salaam.