Na Dickson Bilikwija , JamhuriMedia, Pwani

TIMU ya ukaguzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imemkamata mteja mmoja kwa tuhuma za kufanya uunganishaji haramu wa umeme katika eneo la Kilungule-Camp, Mtaa wa Kaikai, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Tukio hilo limebainika Septemba 4, 2026, wakati timu hiyo ilipokuwa ikifanya ukaguzi wa kawaida wa mita na miunganisho ya umeme katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, mteja anayedaiwa kuhusika na tukio hilo anatambulika kwenye mita kwa jina la Zaitun Mwakalonge, huku wakati wa operesheni hiyo akiwakilishwa na Rose T. Mwenda.

Akizungumza baada ya tukio hilo, Mkaguzi Mkuu wa TANESCO Mkoa wa Rufiji, Rashid Semboga, alisema mtuhumiwa alikutwa akiwa na miunganisho haramu iliyokuwa ikiwezesha nyumba yake kupata umeme bila kupitia kwenye mita.

Semboga alisema hatua zimechukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo, huku akieleza kuwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Alisema baada ya kubaini ukiukwaji huo, miunganisho yote haramu ilikatwa mara moja, huku mteja huyo akipewa fomu ya makosa kwa ajili ya kuanzisha hatua za kisheria.

“Miunganisho yote haramu imekatwa na mteja amepewa fomu ya makosa. Kesi itafunguliwa na uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini iwapo kuna watu wengine waliohusika,” alisema Semboga.

Ukamataji huo umefanyika wakati TANESCO ikiendelea na zoezi la ukaguzi wa mita na miunganisho ya umeme katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kudhibiti vitendo vya wizi wa umeme na matumizi yasiyo halali ya huduma hiyo.

TANESCO imewataka wananchi kutoa taarifa pindi wanapobaini vitendo vya wizi au uunganishaji haramu wa umeme, kupitia namba zake za huduma kwa wateja.

Shirika hilo limeonya kuwa wizi wa umeme ni kosa la jinai linaloweza kusababisha adhabu ikiwemo faini na kifungo, likisisitiza kuwa kulipa bili ya umeme ni rahisi na salama kuliko kukabiliwa na sheria.