Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Watoa huduma za afya nchini wametakiwa kuzingatia maadili, uadilifu, huruma na utu katika kuwahudumia wagonjwa na kuacha mtazamo wa kuona ugonjwa wa mtu ni fursa ya kujipatia fedha.
Rai hiyo imetolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania na Makamu wa Pili wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Nelson Kisare, katika Mkutano Mkuu wa 89 wa Chama cha Madaktari Wakristo Tanzania (TCMA), unaoendelea Jijini Dodoma.
Amesema taaluma ya udaktari ni huduma inayohitaji uaminifu, weledi na kujali utu wa binadamu, hivyo wagonjwa wanapaswa kuhudumiwa kwa haki, upendo na huruma.
Askofu Kisare amesema si sahihi kwa mtoa huduma kumwona mgonjwa anayefika hospitalini kama fursa ya kutengeneza faida binafsi, akisisitiza kuwa “ugonjwa si fursa,” bali ni changamoto inayopaswa kuhudumiwa kwa utu na huruma.
Pia amewataka watoa huduma kuwa waadilifu katika matumizi ya dawa, vifaa tiba na rasilimali nyingine za hospitali, akisema matumizi mabaya yanaweza kudhoofisha ubora wa huduma na kupunguza imani ya wananchi.
Amesema Serikali na wadau wa afya wanapaswa kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, hasa kuhakikisha wananchi kutoka kaya zenye uwezo mdogo wanatambuliwa na kupata huduma kwa urahisi.
Askofu Kisare ameeleza kuwa bado kuna changamoto ya uelewa kuhusu namna kaya maskini zinavyotambuliwa, mahali pa kujiandikisha na huduma zinazolipiwa kupitia mfumo huo.
Akizungumza kuhusu mchango wa taasisi za dini katika sekta ya afya, Rais wa TCMA, Padre Gilbert Sanga, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji katika Hospitali ya Mwambani, Songwe, amesema hospitali na vituo vya afya vinavyomilikiwa na taasisi za dini vimekuwa sehemu muhimu ya mfumo wa afya nchini, hususan katika maeneo ya vijijini.
Amefafanua kuwa Hospitali na vituo vya afya vinavyomilikiwa na taasisi za dini nchini vinatoa takribani asilimia 42 ya huduma za afya nchini hali inayoonyesha mchango wake katika kuimarisha huduma za afya.
Padre Sanga amesema kwa sasa kuna takribani vituo 900 vya afya na hospitali 100 vinavyomilikiwa na taasisi za dini, ambavyo vinaendelea kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za rufaa katika ngazi za mikoa na maeneo mengine.
Amesema TCMA imekuwa ikifanya mikutano kila mwaka tangu kuanzishwa kwake mwaka 1937, huku mkutano wa mwaka huu ukiwa wa 89 na kwamba mkutano huo umejikita katika kujadili namna ya kuboresha huduma zinazotolewa katika vituo vinavyomilikiwa na taasisi za dini, kuimarisha ushirikiano na Serikali na kuweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
Kwa mujibu wa Padre Sanga, utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni miongoni mwa ajenda muhimu za mkutano huo, huku hospitali za taasisi za dini zikiwa katika mchakato wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma kupitia mfumo huo.
Amesema pia afya ya akili mahali pa kazi, imepewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake katika ustawi wa watumishi na ubora wa huduma wanazowapa wananchi.
Naye Katibu Mtendaji wa TCMA na Katibu wa Afya wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Dkt. Paulina Arkard, amesema chama hicho kiko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora bila kujali maeneo wanayoishi au uwezo wao wa kifedha.
Naye Katibu wa Hospitali ya Kirutheri Machame, Kilimanjaro, Blessing Kisanga, amesema mkutano huo unawapa watendaji wa hospitali za taasisi za dini fursa ya kujengewa uwezo kupitia mada za kiroho, afya na uzoefu wa taasisi zilizofanya vizuri.
Hata hivyo, amesema baadhi ya hospitali zilizoingia mikataba na Serikali zinakabiliwa na changamoto ya kupata watumishi mbadala baada ya watumishi wanaolipwa na Serikali kustaafu.
Kisanga amesema hali hiyo husababisha kupungua kwa idadi ya watumishi na kuathiri utoaji wa huduma, hivyo wamekuwa wakihitaji utaratibu wa kupata vibali vya kuajiri watumishi wapya ili hospitali hizo ziendelee kufanya kazi kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Afisa Utawala wa Hospitali ya Mtakatifu Martin, Kilwa Kivinje, Joseph Njenga, amesema changamoto kubwa katika vituo vya afya vilivyopo vijijini ni pamoja na uhaba wa watumishi, dawa, vifaa tiba na vifaa vya maabara.
Amesema Serikali inapaswa kuendelea kuimarisha upatikanaji wa rasilimali hizo ili wananchi wa vijijini wasilazimike kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Pamoja na mambo mengine ,Mkutano Mkuu wa 89 wa TCMA umeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika kuimarisha sekta ya afya, huku washiriki wakieleza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu, dawa, vifaa tiba, afya ya akili na Bima ya Afya kwa Wote ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.






