
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kusimamia Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 08 Septemba 2026, Ikulu Zanzibar, wakati akikabidhiwa Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025 na Mwenyekiti wa ZEC, Mhe. Jaji George Joseph Kazi.
Amesema Serikali na ZEC zinapaswa kuendelea kushirikiana kutatua changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi huo ili zisijirudie katika chaguzi zijazo.
Aidha, ameipongeza ZEC kwa kuongezeka kwa idadi ya wapiga kura walioandikishwa kutoka 566,352 mwaka 2020 hadi 717,557 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 26.7, pamoja na Serikali kugharamia uchaguzi huo kwa asilimia 100 kwa mara ya kwanza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ZEC, Mhe. Jaji George Joseph Kazi, amesema mafanikio mengine ni kuendelea kutumia Tactile Ballot Folder kuwawezesha watu wenye ulemavu wa kuona kupiga kura bila msaada, pamoja na kupatikana kwa jengo la kisasa la One Stop Center na majengo sita ya Afisi za Uchaguzi za Wilaya.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru ZEC kwa kazi iliyofanyika na kuwataka viongozi na watendaji wake kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi, huku Serikali ikiendelea kushirikiana na Tume kuimarisha mazingira ya chaguzi zijazo.










