Mtafiti wa teknolojia ya Akili Mnemba ameyashutumu vikali makampuni ya Marekani kwa kile alichokieleza kama “kucheza na maisha ya watu” wakati yakiunda mifumo ya kompyuta itakayozidi uwezo wa binaadamu.
Jacob Coxon alikuwa mtafiti katika kampuni ya AI ya Anthropic nchini Marekani lakini sasa amejiuzulu. Hatua yake ya kujiuzulu imekuja na onyo hili kali alilolichapisha kupitia mtandao wa X siku ya Jumanne akisema huko siku za usoni AI si tu itakuwa na uwezo wa kudukua kila kitu bali pia itaweza “kuwa na mamlaka halisi pamoja na rasilimali.”
Kulingana na mtafiti huyo, watengenezaji wakubwa wa AI sasa wanaunda mifumo ya kompyuta itakayokuwa na uwezo unaozidi ule wa binaadamu, na kusisitiza kitisho kinachoukabili ulimwengu katika kipindi cha muda mfupi ujao.


