*Watatoa matibabu mbalimbali ya kibingwa
*Itafanyika katika hospitali ya JKCI-ALMC kuanzia tarehe 21
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Hospitali ya JKCI–ALMC Arusha (Selian ya Mjini) imeandaa Kambi Maalum ya Matibabu ya Kibingwa itakayofanyika kuanzia Septemba 21 hadi 24, 2026, ikiwakutanisha madaktari bingwa na wabobezi kutoka Tanzania na India.
Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dkt. Tatizo Waane, alisema jana kuwa kambi hiyo itawakutanisha wataalamu kutoka Apollo Hospitals–India, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) pamoja na madaktari bingwa wa JKCI–ALMC Arusha (Selian ya Mjini).
Alisema kambi hiyo imelenga kuwafikishia wananchi huduma za kibingwa katika maeneo ya magonjwa ya mfumo wa fahamu, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, magonjwa na upasuaji wa mfumo wa mkojo, pamoja na magonjwa, upasuaji wa mifupa, viungo na majeraha.
“Tunatarajia kuona wagonjwa kati ya 100 hadi 200 kwa siku. Watapata nafasi ya kuonana na madaktari bingwa, kufanyiwa tathmini, kupata ushauri wa kitaalamu na kuelekezwa kuhusu hatua zinazofaa za matibabu,” alisema Dkt. Waane.
Alieleza kuwa huduma zitakazotolewa moja kwa moja kupitia kambi hiyo zitakuwa bila malipo, lakini mgonjwa atakayehitaji vipimo, dawa, upasuaji au huduma nyingine za ziada atachangia gharama kulingana na huduma inayohitajika.
Kwa mujibu wa Dkt. Waane, baadhi ya wagonjwa watakaobainika kuwa na matatizo yanayohitaji matibabu ya kina wataandaliwa kwa ajili ya upasuaji au huduma nyingine za kibingwa kulingana na tathmini ya madaktari.
Alitoa wito kwa wananchi wa Arusha na mikoa jirani, ikiwemo Kilimanjaro, Manyara, Singida na maeneo mengine ya Kanda ya Kaskazini, kutumia fursa hiyo kupata huduma za wataalamu waliobobea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba wa JKCI–ALMC Arusha (Selian ya Mjini) na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dkt. Salehe Hamisi Mchete, amesema kambi hiyo ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu zaidi na wananchi.
Alisema pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa, kambi hiyo itatumika kujenga uwezo wa wataalamu wa afya kupitia Mafunzo Endelevu ya Kitabibu (CME) yatakayoshirikisha madaktari bingwa kutoka Tanzania na India.
“Tunataka baada ya kambi hii wagonjwa wapate huduma, lakini pia maarifa yabaki kwa wataalamu wetu. Tutajadili mbinu za kisasa za matibabu, teknolojia mpya za upasuaji na namna bora zaidi ya kuwahudumia wagonjwa,” alisema Dkt. Mchete.
Akizungumza kwa niaba ya timu ya madaktari kutoka Apollo Hospitals–India, Dkt. Mahendra Pal, Daktari Bingwa wa Saratani za Mfumo wa Mkojo (Uro-Oncology), alisema wamefurahishwa kupata nafasi ya kuja Tanzania kufanya kazi pamoja na madaktari bingwa wa hapa nchini.
Dkt. Pal, ambaye amebobea katika saratani za tezi dume, figo, kibofu cha mkojo, korodani na saratani nyingine za mfumo wa mkojo, amesema wataalamu kutoka Apollo watashirikiana na madaktari wa Tanzania katika maeneo ya urology, neurosurgery na orthopaedics.
“Tunafurahi kuja Tanzania na kufanya kazi pamoja na wataalamu wa hapa. Tunawaalika wananchi kutumia fursa hii kuonana na madaktari waliobobea na kupata huduma zinazohitajika,” amesema.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mfumo wa Fahamu kutoka MOI, Dkt. Juma Magogo Mzimbiri, amesema ujio wa wataalamu hao ni fursa muhimu kwa wananchi wa Arusha na Kanda ya Kaskazini kupata huduma za madaktari bingwa wa ndani na nje ya nchi katika eneo moja.
Amesema katika kambi hiyo atashiriki pamoja na Dkt. Remigius Rugakingira, Daktari Bingwa wa Mfumo wa Mkojo kutoka BMH, na Dkt. Emil Urasa, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa na Majeraha kutoka MOI.
“Tunawahimiza wananchi wenye matatizo ya uti wa mgongo, ubongo, kifafa, kiharusi na matatizo mengine ya mfumo wa fahamu kutumia fursa hii. Vilevile wenye matatizo ya mfumo wa mkojo, tezi dume, matatizo ya korodani kwa watoto na baadhi ya changamoto za figo zinazohitaji tathmini ya urology wanakaribishwa,” amesema Dkt. Magogo.
Uongozi wa JKCI–ALMC Arusha (Selian ya Mjini) umetoa wito kwa hospitali na vituo vya afya kuwaelekeza wagonjwa wanaoweza kunufaika na huduma hizo, huku taasisi za afya zikihimizwa kuwawezesha wataalamu wao kushiriki katika mafunzo ya CME.
Kambi hiyo itafanyika JKCI–ALMC Arusha (Selian ya Mjini) kuanzia Septemba 21 hadi 24, 2026.







