Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Jamhuri ya Watu wa China zimesaini Mkataba wa utekelezaji wa ujenzi wa hospitali mpya ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itakayojengwa Mloganzila.

Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam pamoja na kufanya makabidhiano ya vifaa tiba na dawa kutoka kwa timu ya madaktari wa Jamhuri ya Watu wa China ikiwa ni hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China katika sekta ya afya.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe alisema kusainiwa kwa mkataba huo ni ushahidi rasmi kwamba mradi huo umeingia katika hatua mpya ya utekelezaji na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China unavyoendelea kuzaa matokeo yanayogusa moja kwa moja maisha na ustawi wa watanzania.

“Upande wa sekta ya afya sisi tumekuwa wanufaika wakubwa sana wa ushirikiano na Jamhiri ya Watu wa China. Moja ya matokeo yake ni Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo hapo nyuma hatukuwa nayo. Taasisi hii tuliipata kutokana na ushirikiano ambao tumekuwa nao”, alisema Dkt. Magembe

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian alisema China imekuwa mshirika wa Tanzania katika sekta ya afya kwa muda mrefu akitolea mfano JKCI ambayo ilikabidhiwa rasmi kwa Serikali ya Tanzania Septemba 2012 baada ya kujengwa kwa msaada wa China.

“Ninafurahi kuona kwamba baada ya zaidi ya muongo mmoja wa maendeleo taasisi inaendelea kufanya vizuri. Wagonjwa wengi wa Tanzania hawalazimiki tena kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya upasuaji wa moyo bali wanaweza kupata huduma bora za matibabu hapa nchini kwa wakati”, alisema Mingjian

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema ujenzi wa hospitali mpya ya JKCI utaunga mkono mipango ya JKCI kuongeza huduma za kibingwa ikiwemo mpango wa kuanza kutoa huduma za upandikizaji wa moyo (heart transplant) ifikapo mwaka 2030.

“Mradi huu ni matokeo ya ushirikiano mzuri unaofanywa na Tanzania na China ambao ulianza tangu miaka ya sitini. Hospitali itakayojengwa itakuwa na teknolojia ya hali ya juu na itaifanya JKCI kuwa kituo kikubwa cha matibabu na upasuaji wa moyo kwa Afrika Mashariki na Kati”, alisema Dkt. Kisenge.

Ujenzi wa Hospitali mpya ya moyo nchini unatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania katika kutoa huduma bingwa na za kisasa za uchunguzi na matibabu ya moyo pamoja na kuimarisha utaalamu, teknolojia na miundombinu ya huduma za moyo nchini.