SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza kuwa maziko ya Mama Fatma Karume, aliyefariki usiku wa Jumatatu, Septemba 21, 2026, yatafanyika leo Jumanne, Septemba 22, 2026.

Akitoa taarifa ya Serikali kuhusu kifo cha mwanasiasa huyo aliyekuwa mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alisema sala ya maiti itaswaliwa Masjid Jaamiu Zinjibar, Mazizini, baada ya Swala ya Alasiri kwa wanaume, huku wanawake wakiwa katika nyumba ya familia, Mbweni.

Katika taarifa hiyo, Hemed alisema marehemu Mama Fatma atazikwa katika Makaburi ya Familia yaliyopo Mbweni na kwamba SMZ imehuzunishwa na kifo hicho.

Hemed alisema Mama Fatma Karume alikuwa sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar, hasa katika kipindi cha kabla na baada Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Mama Fatma Karume mbali ya kuwa mke wa Hayati Sheikh Karume, anatajwa kuwa ni miongoni mwa viongozi wanawake waliochangia kuimarika kwa ushiriki wa wanawake katika harakati za kudai uhuru wa Zanzibar uliopatikana kupitia Mapinduzi mnano mwaka 1964.

Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mama Fatma alihudumu kama Mama wa Kwanza wa Zanzibar kuanzia mwaka 1964 hadi 1972 huku taarifa za kihistoria zikieleza kuwa alikuwa akishiriki katika shughuli za kuhamasisha wanawake, ikiwemo kupitia Umoja wa Akina Mama wa Afro-Shirazi Party kwa kutembelea maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika ujenzi wa taifa.

Aidha Mama Fatma pia ni mama wa watoto waliokuja kuwa watu mashuhuri katika utumishi wa umma, akiwemo aliyekuwa Rais wa Zanzibar awamu ya 6, Dk. Amani Abeid Karume, aliyeiongoza Zanzibar kuanzia mwaka 2000 hadi 2010, pamoja na Mwanadiplomasia aliyehudumu nchi mbali mbali, Balozi Ali Abeid Amani Karume.

Taarifa za kihistoria zinaeleza kuwa Mama Fatma Karume, alizaliwa Bumbwini, wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, katika familia ya Mzee Gullam Hussein Jamal, aliyewahi kuwa Meya wa Unguja Mjini, aliolewa na marehemu Sheikh Karume mwaka 1944 akiwa na umri wa miaka 15 alishiriki katika harakati za kudai haki za wanawake wakati wa utawala wa kikoloni.

Kumbukumbu zinamtaja kuwa alikuwa miongoni mwa wanawake waliopigania haki ya wanawake kupiga kura, hatua iliyochochea mabadiliko yaliyowezesha wanawake kushiriki katika uchaguzi wa mwaka 1957.

Katika michezo, Mama Karume anatajwa kuhamasisha kuanzishwa kwa vikundi ya michezo na muziki vilivyowaunganisha wananchi na kuchochea kasi ya kudai uhuru na kuhamasisha umoja wa kitaifa baada ya Mapinduzi akijipambanua kuwa ni mmoja ya wanachama na viongozi wa ngazi ya juu wa klabu ya soka ya Yanga ya jijini Dar es salaam.