Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amewaagiza wafugaji mkoani humo kuacha mara moja kuingiza na kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia uharibifu wa mazao unaosababishwa na mifugo.
Ametoa agizo hilo Septemba 22, 2026, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi katika Halmashauri za Mji wa Rufiji na Kibiti, ambako amesikiliza kero na malalamiko mbalimbali ya wananchi na kutoa maelekezo ya hatua za kuchukuliwa.
Alisema Serikali haiwezi kuendelea kushuhudia mazao ya wakulima yakiharibiwa na mifugo, wakati tayari maeneo yametengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji, hivyo kila kundi linapaswa kuheshimu maeneo lililotengewa na kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria.
“Hatukubali kuendelea kuona mazao ya wakulima yakiharibiwa wakati kila kundi limetengewa maeneo kwa ajili ya shughuli zake, wafugaji waheshimu maeneo ya wakulima na waache mara moja kuingiza mifugo kwenye mashamba,” alieleza Nyongo.
Aidha, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Rufiji kusimamia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo na kuhakikisha mfugaji yeyote atakayebainika kuingiza ama kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima anakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, Nyongo ameipongeza Halmashauri ya Rufiji kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuvuka malengo yaliyowekwa, huku akizitaka Halmashauri za Rufiji na Kibiti kuendelea kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato ili kuongeza uwezo wa Serikali za mitaa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kuhusu utabiri wa mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha kwa kiwango kikubwa, Mkuu huyo wa Mkoa alizitaka Halmashauri zote kuimarisha maandalizi na kuchukua hatua za tahadhari mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Aliwataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni na maeneo mengine hatarishi kuhama mapema na kuhamia maeneo salama, akisisitiza kuwa usalama wa maisha ya wananchi unapaswa kupewa kipaumbele.
Vilevile, Wakuu wa Wilaya za Rufiji na Kibiti kuanza kutambua na kuainisha maeneo salama yatakayotumika kuhifadhi wananchi watakaoweza kuathiriwa na mvua hizo, pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana katika maeneo hayo.
Ziara hiyo ni ya kwanza ya kikazi kwa Nyongo katika Halmashauri za Mkoa wa Pwani tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa huo, ikiwa na lengo la kujitambulisha, kusikiliza kero za wananchi na kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika maeneo hayo.




