Na Asia Singano, WF -Arusha
Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Wizara ya Fedha, Mhandisi Kenneth Nindie, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa vihatarishi pamoja na kujenga uwezo wa wataalam wa ukaguzi wa ndani ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika taasisi za umma.
Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa 19 wa Ukaguzi kwa ngazi ya utawala, Mhandisi Nindie alisema, kuimarika kwa usimamizi wa vihatarishi kunahitaji mifumo madhubuti, uendelezaji wa ujuzi na matumizi ya fursa za mafunzo yanayopatikana, ikiwemo mafunzo yanayotolewa kwa njia ya mtandao.
Alisema Wizara ya Fedha inatambua umuhimu wa kuendelea kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa ndani yatakayowawezesha wataalam kuongeza ujuzi wao, hatua inayoweza kusaidia kuimarisha uwezo wa taasisi katika kutambua na kudhibiti vihatarishi.
‘’Tunategemea kuwa na mafunzo kwa njia ya mtandao ili kuongeza uwezo wa wakaguzi wa ndani, na kwa wakaguzi ambao tumeshiriki na tupo basi mijadala hii ambayo imeendelea jana na leo itusaidie kuona kuwa Bodi zetu zinahitaji tufanye nini lakini taasisi kufikia malengo ambayo tumejiwekea hasa kuhakikisha thamani ya mali za umma inapatikana kwa wananchi ambao tunawatumikia’’alisema Mhandisi Nindie.
Alisema ushirikiano kati ya bodi, menejimenti, wakaguzi wa ndani na wadau wengine ni muhimu katika kuhakikisha mapendekezo yanayotokana na ukaguzi yanafanyiwa kazi na kusaidia kuboresha utendaji wa taasisi.
‘’Tutaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote katika kuimarisha mifumo ya ukaguzi wa ndani lakini usimamizi wa vihatarishi ili kuongeza tija na ufanisi kwa lengo moja kubwa la kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa tija ili kuchagia maendeleo ya Taifa’’ alisema Mhandisi Nindie.
Katika mkutano huo viongozi mbalimbali wa Wizara ya Fedha, walishiriki akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda.
Katika mkutano wa 19 wa Mwaka wa Ukaguzi wa Ndani kwa ngazi ya Utawala ambao umehitimishwa rasmi ambapo washiriki walipata fursa ya kujadiliana kubadilishana uzoefu pamoja na mafunzo mbalimbali ikiwemo matumizi ya teknolojia hususan matumizi ya Akili Unde (AI), huku wakisisitizwa kushiriki katika kujadili na kusimamia hatari na athari za teknolojia hiyo kabla ya kuangalia manufaa yake pekee.













