Na OWM–TAMISEMI, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ametoa maagizo kwa Mkurugenzi anayeshughulikia Mipango Miji na Vijiji wa OWM–TAMISEMI, Kamishna wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara hiyo na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kuchambua hoja zaidi ya 60 zilizowasilishwa na wananchi 22 kuhusu mgogoro wa muda mrefu wa mipaka ya kiutawala na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi, ndani ya siku 14 na kuwasilisha taarifa ya uchambuzi huo.

Prof. Shemdoe amesema baada ya kupokea taarifa hiyo, itawasilishwa kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ambaye atawasilisha hoja na maombi ya wananchi kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kupata maelekezo ya utatuzi wa kudumu wa mgogoro huo.

Prof. Shemdoe ametoa agizo hilo Septemba 23, 2026, wakati wa mkutano na wananchi hao uliofanyika katika viwanja vya Chanika Zingiziwa, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais aliyoyatoa Septemba 18, 2026 akiwa Dampo la Pugu, akiwataka Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Waziri wa Maliasili na Utalii kukutana na wananchi hao ndani ya siku saba ili kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

“Taarifa ya uchambuzi huo itatuwezesha sisi Mawaziri kwenda kwenye eneo la mgogoro kupitia alama za mipaka (beacon) ili kujiridhisha na taarifa zilizotolewa na wananchi hao na hali halisi ya eneo la mgogoro wa mipaka ya kiutawala,” amesema Prof. Shemdoe.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amewashukuru wananchi waliowasilisha taarifa na waliohudhuria mkutano huo, akiwahakikishia kuwa watendaji wa Wizara yake wako tayari kutekeleza maelekezo yatakayotolewa na mamlaka.

Dkt. Akwilapo amesema watendaji hao watafanya kazi kwa uadilifu na weledi katika kutekeleza maelekezo yatakayotolewa na mamlaka kuhusu utatuzi wa mgogoro huo, kwa lengo la kuleta tabasamu kwa wananchi.

Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, amesema hatua ya kuwasikiliza wananchi wenye changamoto ya mipaka ya kiutawala na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi ni utekelezaji wa falsafa ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusikiliza kero na changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi, na kuongeza kuwa anaamini mamlaka zitatoa suluhisho sahihi kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Hatua hiyo inaakisi msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kusikiliza wananchi, kusimamia haki na kutatua changamoto zao kwa vitendo, ikiwemo kuhakikisha masuala ya ardhi yanasimamiwa kwa haki na usawa, migogoro inatatuliwa kwa kuzingatia sheria na ukweli wa maeneo husika, huku mifumo ya upangaji, upimaji na umilikishaji ikiendelea kuimarishwa ili kuzuia migogoro.