Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
SERIKALI imeanza kuchunguza waajiri wanaodaiwa kutumia taarifa na akaunti za watumishi kuombea mikopo binafsi bila ridhaa yao, huku ikionya kuwa watakaobainika kukiuka sheria na taratibu watachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.
Hatua hiyo inalenga kuwalinda watumishi dhidi ya kubebeshwa madeni na majukumu ya kifedha ambayo hawakuomba wala kuyakubali.
Kauli hiyo imetolewa October 7,2026 na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, jijini Dodoma wakati Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ukiendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa rasilimali watu na wahasibu kutoka wizara na taasisi za umma nchini.
Mkomi amesema matumizi ya taarifa au akaunti za watumishi katika kuomba mikopo bila ridhaa yao ni ukiukwaji wa sheria na taratibu za utumishi, akisisitiza kuwa Serikali haitawavumilia waajiri wanaotumia nafasi zao kuwanufaisha watumishi kwa maslahi binafsi.
“Tunaanza kufuatilia mnyororo mzima wa waajiri wanaofanya mambo haya, atakayebainika amevunja sheria na taratibu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema.
Amesema vitendo hivyo vinaweza kuwaweka watumishi katika mazingira magumu kifedha, ikiwemo kubebeshwa madeni ambayo hawakuyakubali, hali inayoweza kuathiri ustawi wao na utekelezaji wa majukumu yao.
Mkomi amewataka waajiri kuhakikisha wanaheshimu haki, utu na maslahi ya watumishi wanaowaongoza, akisisitiza kuwa mamlaka waliyonayo mahali pa kazi hayapaswi kutumiwa kinyume cha sheria na taratibu.
Katika hatua nyingine, Mkomi ameitaka WCF kuendelea kutathmini uwezekano wa kupanua wigo wa fidia kwa wafanyakazi wanaopata madhara mbalimbali yanayohusiana na mazingira ya kazi.
Amesema kuna umuhimu wa kuangalia kwa mapana changamoto za kiafya zinazoweza kuwakabili wafanyakazi na kutathmini namna wanavyoweza kupata msaada na huduma stahiki.
Ametaja pia umuhimu wa kuangalia changamoto kama shinikizo la damu, ili kubaini namna wafanyakazi wanaokabiliwa na hali hiyo wanavyoweza kusaidiwa kulingana na taratibu na mfumo wa fidia.
Aidha, amewaonya waajiri wanaowatelekeza watumishi wanapokuwa hospitalini baada ya kupata madhara yanayohusiana na kazi, akisisitiza kuwa wana wajibu wa kuhakikisha taarifa kuhusu madhara hayo zinawasilishwa katika maeneo husika kwa wakati.
Amesema uwasilishaji wa taarifa kwa wakati ni muhimu kwa mfanyakazi kupata haki na msaada unaostahili bila kuchelewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, amesema shughuli zinazotekelezwa na mfuko huo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuhakikisha ustawi wa wananchi unakuwa jumuishi.
Dkt. Mduma amesema WCF inalenga kuhakikisha wafanyakazi wanaopata madhara kutokana na ajali au magonjwa yanayotokana na kazi hawasahauliki katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.
Amesema mfuko huo utaendelea kusimamia misingi ya ustawi, haki na usawa kwa wafanyakazi, akieleza kuwa misingi hiyo ni sehemu muhimu ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Lengo letu ni kuhakikisha mfanyakazi anayepata madhara yanayotokana na mazingira ya kazi anapata haki na huduma stahiki kwa wakati, ili asiwe nyuma katika kunufaika na maendeleo ya Taifa,” amesema Dkt. Mduma.





