Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songea
Shule ya Sekondari ya Kata ya Zimanimoto, iliyopo kata ya Misufini katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imepata matumaini mapya katika kukabiliana na changamoto ya maji baada ya mdau wa maendeleo ya elimu, Bi. Getrude Haule, kuchangia vifaa vya miundombinu ya maji vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni mbili.
Msaada huo unalenga kuwezesha shule hiyo kupata huduma ya maji kwa uhakika na hivyo kupunguza changamoto iliyokuwa ikiikabili shule hiyo toka kuanzishwa 2007.
Vifaa hivyo vinatarajiwa kukamilisha miundombinu ya maji na kusaidia wanafunzi pamoja na walimu kupata huduma hiyo kwa urahisi ndani ya mazingira ya shule.
Bi. Haule ambaye ni mgeni rasmi katika mahafari ya kidato cha nne yaliyofanyika Jana shuleni hapo alisema kuwa ameamua kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, akiamini kuwa upatikanaji wa maji ni sehemu muhimu ya kuhakikisha wanafunzi wanajifunza katika mazingira salama na rafiki.
Hata hivyo amempongeza Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa wa kuboresha mazingira ya shule za sekondari za kata jambo ambalo limeongeza ufaulu kwa wanafunzi wanaomaliza shule hizo tofauti na hapo awali.
Mbali na changamoto ya maji, shule hiyo pia inakabiliwa na uhitaji wa darasa maalumu kwa ajili ya kufundishia somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), jambo linaloonyesha umuhimu wa wadau kuendelea kushirikiana na shule katika kuboresha miundombinu ya elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo ya Sekondari ya Zimanimoto Mwalimu Damian Mahuve ameeleza kuwa mchango huo ni hatua muhimu katika kutatua changamoto ya maji na amemshukuru Bi. Haule kwa kujitolea kuunga mkono maendeleo ya elimu shuleni hapo na kuwaomba wadau wengine wa elimu kuwa na moyo wa kujitolea ili kuboresha zaidi mazingira ya kufundishia.
Alisema kuwa Msaada huo unatarajiwa kuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa jamii ya shule ya Zimanimoto na si vinginevyo.




