Na Joe Beda Rupia, JmahuriMedia, Dar es Salaam

Aiseee! Kesho ni Oktoba 14. Miaka 27 imetimia sasa tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipoiaga dunia. Kila mwaka tunamkumbuka kwa hotuba, picha, nyimbo na maneno yake yaliyogeuka kama dira na mithali za taifa.

Ndiyo. Tanzania ni taifa lake. Tanzania ni ya Mwalimu Nyerere.

Lakini mimi ninajiuliza au huwa ninajiuliza mara kwa mara. Hivi, lile shauri la kumtangaza Mwalimu kuwa Mtakatifu limefikia wapi? Linaendeleaje? Au ni siri ya Kanisa Katoliki?

Nisieleweke vibaya. Siulizi kwa sababu nina haraka ya kuona sanamu au picha zake ndani ya makanisa na hata altareni. Wala sitaki kumfundisha Papa Leo XIV kazi au wasaidizi wake, hasa Baba Askofu Msonganzila wa Jimbo la Musoma na Baba Askofu Mkuu Luwaichi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Mimi ni muumini mwenye maswali, na kuuliza si dhambi!

Miaka kadhaa iliyopita niliandika makala niliyoipa kichwa cha habari; ‘Vita ya Kagera na Utakatifu wa Nyerere’. Nilikuwa nikijiuliza iwapo baadhi ya uamuzi wa Mwalimu wakati wa vita dhidi ya Idi Amin unaweza kutusaidia kuuelewa ‘utu’ wake; au niseme upande wa pili wa ‘utakatifu’ wake.

Leo ninairudia hoja hiyo hiyo. Tena kwa sababu kubwa zaidi; kwamba huyu baba alikuwa na kipaji cha ajabu sana!

Hebu fikiria. Alikuwa mwalimu, mwanasiasa, mwanafalsafa, mtafsiri na msomaji wa maandiko matakatifu. Huyu jamaa alifikia hata kutafsiri maandiko ya Biblia kwa Kizanaki! Yaani, Injili na masomo ya Jumapili.

Huenda alitamani Wazanaki wote wapate Habari Njema ya Wokovu. Sijui alifanikiwa kwa kiasi gani, lakini jitihada zake hizi zinaweza kuwashawishi ‘wakubwa’ kumtakatifuza.

Alitafsiri pia kazi za William Shakespeare kwa Kiswahili. Baadaye akaandika tenzi za Injili. Asieee! Sisi wengine kutafsiri tu ujumbe wa Kiingereza wa WhatsApp tunahitaji kamusi, yeye alikuwa akipambana na Shakespeare na Mtume Paulo!

Sawa, ni kweli kwamba kipaji si utakatifu. Hata shetani, kwa mujibu wa mafundisho ya dini, ana maarifa yake. Kanisa halimtakatifuzi mtu kwa sababu alikuwa na akili nyingi, aliongoza taifa au aliandika vitabu.

Linachunguza maisha yake, imani, maadili na ushahidi wa namna alivyoishi.

Kwa sasa, katika mchakato huo, Nyerere anatambuliwa kama ‘Mtumishi wa Mungu’. Hiyo si sawa na ‘Mwenyeheri’, wala si sawa na ‘Mtakatifu’. Mchakato huu una taratibu zake. Hatua kwa hatua. Mtumishi wa Mungu ni hatua ya kwanza.

Na Kanisa halina tabia ya kupitisha majina kwa kupiga kura za mashabiki!

KWA HABARI ZAIDI ZA KINA SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 13- 19, 2026