Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Kibaha
Malalamiko ya magonjwa kwa watoto, vifo vya mifugo, uharibifu wa mazao na kutiririshwa kwa maji machafu kwenye makazi ya watu yameibua hofu miongoni mwa wakazi wa Kata ya Picha ya Ndege, Kibaha mkoani Pwani, wanaodai shughuli za baadhi ya viwanda zimegeuka tishio kwa maisha yao.
Wananchi hao wanasema maji machafu, vumbi, moshi na mabaki ya kemikali wanazodai kuwa salfa vimekuwa vikisambaa kwenye makazi yao, huku juhudi za kutafuta ufumbuzi kupitia viongozi wa serikali za mitaa na wilaya zikishindwa kuondoa kero hizo.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa malalamiko hayo yanaendelea wakati Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) likiwa limefanya ukaguzi wa viwanda na maeneo mengine ya uzalishaji Kibaha na kubaini upungufu katika usimamizi wa mazingira kwenye baadhi yake.
Hata hivyo, hakuna matokeo ya vipimo vya kitaalamu yaliyowasilishwa kuthibitisha kwamba magonjwa na vifo vya mifugo vinavyolalamikiwa vimesababishwa moja kwa moja na kemikali kutoka viwandani.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wananchi wameiomba serikali kuingilia kati kwa kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha shughuli za viwanda haziathiri afya, mali na mazingira yao.
Maji machafu yazua hofu
Mkazi wa eneo hilo, Baraka Juma, amesema baadhi ya viwanda vinadaiwa kutiririsha maji machafu yaliyochanganyika na taka na mabaki ya kemikali kwenye makazi ya watu.
“Maji hayo yanamwagwa kwenye makazi yetu. Moshi, vumbi na salfa navyo vimekuwa tatizo kubwa, kwetu sisi tunahisi uwekezaji unaotakiwa kutuletea maendeleo lakini sasa unageuka kuwa mateso, tunaiomba serikali itusaidie,” amesema.
Mkazi mwingine, Mariam Bernard, amesema watoto wamekuwa wakikabiliwa na matatizo ya kukohoa, vipele na magonjwa ya kifua, hali ambayo anaihofia kuwa inachangiwa na mazingira yanayowazunguka.
“Watoto wetu wanarudi nyumbani wakiwa wamejaa vumbi, wanapita kwenye vumbi la uchafu wa mabaki ya makaa ya mawe, wanaumwa vifua, wanakohoa mara kwa mara na wengine wanapata vipele wanapocheza kwenye maji hayo.
“Wakati wa kumwaga maji machafu wanafungulia kwenda kwenye makazi ya watu, hata kula kunakuwa vigumu kutokana na harufu inayotoka huko, yaani hiki kitu ni hatari mno,” amesema.
KWA HABARI ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI OKTOBA 13 – 19, 2026



