*Mjadala washika kasi, Serikali yatoa ufafanuzi bila kumtaja mtoa kauli
* ACT yasisitiza Katiba kufuatwa, ADC yataka mipaka iheshimiwe
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedi, Dar es Salaam
Wakati mjadala kuhusu kauli kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho kinachomiliki vyombo vya ulinzi na usalama ukiendelea kuzua maswali, serikali imetoa ufafanuzi kuhusu nafasi ya vyombo hivyo katika taifa.
Aliyetoa ufafanuzi huo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, mwanasheria aliyewahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye bila kumtaja mwanzilishi wa mjadala, amesema: “vyombo vya dola ni vya Watanzania wote.”
Kauli ya Profesa Kabudi imekuja baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Idara ya Oganaizesheni, Paul Chacha, kudai kuwa vyombo vya ulinzi na usalama ni mali ya chama hicho, matamshi yaliyoibua maswali kuhusu tofauti kati ya chama kinachounda serikali na taasisi za dola.
Akizungumza Septemba 26, mwaka huu, mkoani Iringa, Chacha alisema:
“Nani ambaye hajui vyombo vyote vya ulinzi na usalama ni mali ya CCM? Nani hajui mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mali ya CCM? Nani hajui Waziri wa Ulinzi ni mali ya CCM?”
Hata hivyo, takriban siku 10 baadaye, yaani Oktoba 7, mwaka huu, siku moja tu baada ya Gazeti la JAMHURI kuandika kwa kina kauli ya Chacha, akizungumza katika Baraza la Vyama vya Siasa jijini Dar es Salaam, Profesa Kabudi ametoa kauli inayoweka wazi nafasi ya vyombo hivyo kwa wananchi wote.
“Vyombo vya dola ni vya Watanzania wote, ndiyo maana mmefanya vizuri kumwita Kamanda wa Polisi hapa katika Baraza la Vyama vya Siasa. Maana yake vyombo vyote hapa ni vyetu sisi sote,” amesema.
Wakati Profesa Kabudi akisisitiza umuhimu wa mawasiliano kati ya vyama vya siasa na vyombo vya ulinzi na usalama, wachambuzi na viongozi wa vyama vya upinzani wameelekeza mjadala katika wajibu wa kikatiba wa taasisi hizo na namna zinavyotekeleza majukumu yake.
Nini maana ya ‘vyombo vya dola’?
Katika matumizi ya kisiasa na kitaaluma, dhana ya vyombo vya dola ni pana kuliko vyombo vya ulinzi na usalama pekee. Inahusu taasisi zinazoundwa au kutambuliwa kwa mujibu wa Katiba na sheria ili kutekeleza mamlaka na majukumu ya serikali na taifa.
Taasisi hizo zinajumuisha vyombo vya ulinzi na usalama, lakini dola yenyewe ina muundo mpana unaohusisha mamlaka za utendaji, utungaji wa sheria na utoaji haki.
Ni muhimu kutofautisha dola, serikali na chama cha siasa. Dola inaendelea kuwapo hata pale viongozi wa serikali wanapobadilika, wakati chama cha siasa kinaweza kupata au kupoteza mamlaka ya kuunda serikali kupitia uchaguzi.
Katika mjadala wa sasa, hoja kubwa inahusu hasa vyombo vya ulinzi na usalama, vikiwamo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
KWA HABARI ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 13- 19, 2026

