Na Mwandishi Wetu, Sumbawanga
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Rukwa imetumia zaidi ya shilingi milioni 285 kuwawezesha vijana kupitia Mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara kwa kutumia Vikundi vya Kijamii (CBRM).
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA mkoa wa Rukwa Mhandisi Chacha Moseti katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya shule ya msingi Ndua Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Mhandisi Moseti amesema kuwa kiasi hicho cha pesa ni sehemu ya shilingi milioni 516 iliyotengwa kutekeleza shughuli hiyo katika mwaka wa fedha 2026/27.
”Katika mwaka wa fedha 2026/27 tumetenga jumla ya shilingi milioni 516 kwa ajili ya vikundi maalum. Vikundi tulivyonavyo mpaka sasa ni 38 kati ya vikundi hivyo vikundi 21 ambavyo ni sawa na 55% ni vikundi vinavyotokana na vijana na tayari vimeshapatiwa mikataba ya kufanya matengenezo ambayo ina thamani ya shilingi milioni 285″, amefafanua Mhandisi Moseti.
Akielezea umuhimu wa mpango huo kwa vijana na makundi maalum kwa ujumla, Mhandisi Moseti amesema kwamba fedha zinazotolewa kwa makundi hayo kupitia mpango wa CBRM zinawasaidia kujenga mazingira ya wao kuzimiliki barabara zao katika maeneo yao lakini pia zinawasaidia kuongeza kipato kwa ajili ya kuwasaidia wao na familia zao.
”Serikali inatengeneza mazingira ambayo ni wezeshi kwa vijana ili waweze kunufaika na matengenezo ya barabara ambayo yanafanyika kupitia TARURA”, ameongeza Mhandisi Moseti.
Kwa upande wake, Msimamizi Msaidizi wa CBRM mkoa wa Rukwa Mhandisi Abdulrazak Mshana amesema pamoja na faida nyingine lakini mpango huo kwanza unawapa ajira vijana sambamba na kuwaweka katika mfumo rasmi kwa maana kwamba vikundi vyao vinakuwa kama wakandarasi isipokuwa wenyewe wanapatikana katika maeneo ambayo barabara husika zinapita.
Ameongeza kuwa vikundi kuwa katika mfumo rasmi ina maana kuwa vikundi hivyo vinasajiliwa pia vinapitia mfumo wa kawaida wa kuomba zabuni kupitia NEST chini ya Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA).
Naye, Bw. Florence Clonele ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi cha Youth Vision Fighters ambacho kimepata zabuni ya kuhudumia barabara ya Pito-Maragano (km 5) na Bi. Justina Malosko Mwenyekiti wa kikundi cha Wafugaji kuku wanaohudumia barabara ya Kisiwani-Kichangani (km 5) Manispaa ya Sumbawanga wameelezea manufaa wanayoyapata kuwa ni pamoja na kuwaongezea kipato kinachowawezesha kuendesha familia zao.






