Papa Leo XIV alitarajiwa kulazwa katika hospitali ya Roma Jumanne kwa ajili ya kuondolewa uvimbe kwenye mapafu katika upasuaji ambao wataalam wanasema utaamua kama uvimbe huo unaweza kutolewa na ikiwa matibabu mengine zaidi yanahitajika.
Leo ametoa uwazi wa nadra kuhusu tatizo kubwa la kwanza la kiafya kumuhusu hadharani tangu alipochaguliwa kuwa Papa miezi 17 iliyopita.
Alifichua kuhusu ugunduzi wa uvimbe huo mdogo wakati wa sala yake ya Jumapili adhuhuri na kutangaza kwamba anataka uondolewe.
Mamlaka ya Vatican ilisema Papa Leo XIV angelazwa katika hospitali ya Gemelli Jumanne asubuhi, lakini hakukuwa na taarifa kuhusu muda wa upasuaji wenyewe.
Upasuaji huo, ambao kwa kawaida hufanywa mtu akiwa amepigwa ganzi ya jumla (mwili mzima), utahitaji kukaa hospitalini kwa wiki moja na Vatican siku ya Jumatatu ilifuta mikutano ya hadhila ya Papa hadi Oktoba 20.
“Haya ni mambo ambayo yanaweza kutibiwa vizuri sana, ikiwa maneno aliyotumia yanaakisi hali ya kimatibabu,” alisema Dkt. Lorenzo Spaggiari, mkurugenzi wa upasuaji wa kifua katika Taasisi ya Ulaya ya matibabu ya saratani (EIO), ambaye hahusiki na Matibabu ya Papa lakini anayeifahamu timu ya madaktari ya hospitali ya Gemelli.
Spaggiari alisema anatarajia timu ya Gemelli ingefanya uchunguzi wa biopsy ili kubaini kama Leo ana saratani ya mapafu ikifuatiwa na kuondolewa kwa sehemu ya mapafu iliyo na uvimbe.
Uchunguzi wote unaweza kufanywa kwa kutumia mbinu za roboti, na unaweza kufanywa mfululizo, huku mgonjwa amepigwa sindano ya ganzi, na timu tofauti za wataalamu, Spaggiari alisema.

