WAHITIMU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wametakiwa kuzingatia maadili ya Kitanzania na Kiafrika, kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa pamoja na kutumia elimu waliyoipata kujenga jamii yenye uwajibikaji na kuheshimu maslahi ya pamoja.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya 56 ya chuo hicho, akisisitiza kuwa wahitimu wana wajibu wa kulinda tunu za Taifa huku wakitumia maarifa na ujuzi wao kuchangia maendeleo ya nchi.
Amesema Tanzania imeendelea kuheshimika kutokana na misingi ya utu, staha, mshikamano na kujali maslahi ya pamoja, hivyo wahitimu wanapaswa kupokea maarifa na teknolojia mpya bila kupoteza misingi hiyo ya kimaadili.
“Kumbukeni, Watanzania hatuna nchi nyingine ila Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunao wajibu wa kulinda amani, umoja na mshikamano wetu; uhuru wa Taifa letu; Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar; na Muungano wetu,” amesema.
Amesisitiza kuwa elimu waliyoipata wahitimu inapaswa kuonekana kupitia fikra, utendaji, maadili na matokeo chanya wanayoyazalisha katika maeneo yao ya kazi na katika jamii kwa ujumla.
Aidha, amewataka wahitimu kutumia elimu yao kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla, akibainisha kuwa elimu si njia ya kujitenga na jamii, bali ni dhamana inayopaswa kutumika kuitumikia na kutatua changamoto zinazoikabili.
Akirejea ujumbe wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika kitabu chake Uhuru na Maendeleo (1973), amesema elimu inapaswa kuwa msingi wa uwajibikaji na usawa katika jamii, badala ya kuwa nyenzo ya kujipatia manufaa binafsi kwa gharama ya wananchi wengine.
Pia, amewataka wahitimu kuwa na nidhamu, uadilifu na moyo wa huduma, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya utumishi wanapojiunga na sekta ya umma au binafsi.
Amesema vijana wana nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia ujasiriamali, kilimo-biashara, uchumi wa kidijitali, tafiti, ubunifu na huduma za kitaalamu, hasa pale wanapotumia maarifa yao kutatua changamoto za jamii.
Akizungumzia mchango wa Serikali katika elimu ya juu, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuimarisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hususan katika mafunzo, stahiki za watumishi na uendeshaji wa chuo hicho.




