Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa namna ilivyojipanga kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma za kimahakama bila kukatizwa wakati wa mvua za El Niño.

Mhe. Ulega ameyasema hayo Oktoba 12, 2026, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania  jijini  Dodoma, alipofanya ziara ya kujitambulisha katika Mahakama Kuu ya Tanzania na kukutana na  Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, Mtendaji Mkuu wa Mahakama Dkt. John Jingu na viongozi mbalimbali wa Mahakama.

Katika kikao hicho, Jaji Masaju, alimpongeza Mhe. Ulega kwa kuendelea kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  na kumteua kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, ambapo alimkaribisha rasmi na kumweleza kuhusu masuala  ya kiutendaji  kati  ya Wizara ya Katiba na Sheria na Mahakama ya Tanzania.

Akielezea maandalizi ya Mahakama kukabiliana na mvua hizo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Jingu, alisema Mahakama imeweka mazingira bora ya kuwahudumia wananchi katika kipindi chote cha El Niño. Ameeleza kuwa, Mahakama imeandaa mikakati madhubuti ya dharura kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza ikiwemo matumizi ya teknolojia  katika  kuhakikisha Wananchi wanapata Haki zao kwa wakati na kwa urahisi.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Masaju aliipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi, zikiwemo huduma za msaada wa kisheria na programu mbalimbali ikiwemo Sema na Waziri ambapo Wananchi  hupiga  simu katika  Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Wizara na kuwasilisha malalamiko yanayohitaji Msaada wa Kisheria.

Akizungumza baada ya mapokezi hayo, Waziri Ulega alishukuru uongozi wa Mahakama kwa mapokezi mazuri na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Wizara na Mahakama ili kuimarisha utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Alieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma za kisheria na kimahakama kwa wakati, ikiwemo katika vipindi  vya majanga kama El Niño ambavyo vinaweza  kuathiri utoaji wa huduma kutokana na changamoto za  hali  ya hewa.