Na Mwandishi Maalumu, Mwanza

Huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) zimedhihirisha kuwa na uhitaji mkubwa kwa wananchi katika kile mkoa ambapo taasisi hiyo imekuwa ikifanya kambi maalumu za matibabu.

Hayo yamesemwa na Mbunge wa jimbo la Nyamagana Mhe. John Nzilanyingi alipotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya binadamu inayofanyika katika viwanja vya Nyamagana vilivyopo jijini Mwanza.

Mhe. Nzilanyingi alisema kambi hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Nyamagana kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imeonesha namna ambavyo wananchi wa Mwanza wana imani na huduma zinazotolewa na JKCI kwa kuonesha uhitaji mkubwa wa kutaka kupima moyo.

“Naipongeza JKCI kwa kazi nzuri inayofanya ya kuwahudumia wananchi wa kila hali, foleni tunayoiona hapa ikisubiri kupata huduma katika banda la JKCI ni ishara ya imani ya wananchi waliyonayo kwa taasisi hii kutokana na huduma bora wanayoitoa”, alisema Mhe. Nzilanyingi.

Kwa upande wake mwananchi aliyepata huduma katika banda la JKCI aliishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwachagua viongozi wanaojali wananchi na kuwapa fursa ya kuchunguza afya zao bila malipo karibu na maeneo wanayoishi.

Salma Mbusu mkazi wa Mwanza alisema uwepo wa JKCI katika kambi hiyo kumwemwezesha kupima moyo wake, kuyafahamu vizuri magonjwa ya moyo na kuanza kuchukua hatua dhidi ya magonjwa hayo.

“Ninamshukuru Mungu kwa kupata huduma ya kuchunguza moyo wangu nilikuwa na matatizo ya muda mrefu lakini leo nimepata nafasi ya kupima na kufahamu hali yangu ya afya. Nimehudumiwa vizuri na kila kitu kimeenda vizuri”, alisema Salma.

Kambi hiyo maalumu ya matibabu ya magonjwa ya binadamu inayofanyika mkoani Mwanza ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na kuhamasisha jamii kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini mapema matatizo yanayoweza kuathiri afya zao.