Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imezindua kampeni ya Code Plus 255, Twende Tu Utalii, inayolenga kuhamasisha Watanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini na kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia matumizi ya huduma zinazotolewa na wadau wa ndani.

Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Theresia Mugobi, amesema kampeni hiyo itatekelezwa kwa miezi mitatu kuanzia Oktoba 27, 2026 hadi Januari 15, 2027

Itatumian kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka mpya kuhamasisha wananchi kusafiri na kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii.

Amesema kampeni hiyo itahusisha hifadhi za taifa, maeneo ya uhifadhi,makumbusho, maeneo ya kihistoria, misitu, milima,maziwa na fukwe, pamoja na matukio ya kitamaduni, sanaa na michezo.

Utalii hauishii kwenye vivutio vya asili pekee, bali unajumuisha pia matukio mbalimbali yanayovutia watu kusafiri na kutumia huduma za maeneo husika*amesema

Theresia amesema TTB itashirikiana na sekta binafsi, vyama vya watoa huduma za utalii na usafirishaji, watu mashuhuri na watengeneza maudhui kuongeza uhamasishaji, huku kampeni hiyo ikijumuisha ofa na vifurushi maalumu vitakavyowawezesha Watanzania kutalii kwa gharama zinazofikika.

Ameongeza wananchi watapata taarifa za fursa hizo kupitia misimbo ya QR itakayowaelekeza kwenye taarifa za ofa zinazotolewa na wadau wa utalii.

Kwa upande wake, Mbazi Mjema, mwakilishi wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), amesema wamiliki wa mabasi wako tayari kushirikiana na TTB kutangaza utalii wa ndani kupitia vyombo vya usafiri, ikiwemo mabasi yanayofanya safari mbalimbali nchini, ili kuwafikishia wananchi taarifa kuhusu vivutio na fursa za utalii.

Mwigizaji Leah Mwendamseke, maarufu Lamata, amesema kupitia ushawishi walionao wataendelea kutangaza utalii wa ndani, huku wao wenyewe wakiwa mfano kwa kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii nchini na kuhamasisha wananchi wengine kufanya hivyo.

Maxwell Alfred, maarufu Mzee Shayo, amesema Watanzania wanapaswa kutumia fursa ya utalii wa ndani kwasababu gharama za kutembelea vivutio ni nafuu ikilinganishwa na viwango vinavyotozwa kwa watalii wa nje.