Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

WAZIRI wa Sheria na Katiba, Abdallah Ulega, amesema kampeni ya Samia Legal Aid ni mkombozi kwa wananchi wanyonge, kwa kuwa inawezesha kupata huduma za msaada wa kisheria bila malipo, hususan wanaoishi vijijini na maeneo ya pembezoni, ili wafahamu na waweze kudai haki zao kwa mujibu wa sheria.

Aidha ameeleza kuwa Wilaya ya Mafia haipaswi kuachwa nyuma katika utekelezaji wa kampeni hiyo, akieleza kuwa ni sehemu ya Mkoa wa Pwani na hivyo wataalamu wa sheria wanapaswa kufika kutoa huduma kwa wananchi wake.

Akifungua kampeni ya Samia Legal Aid awamu ya pili mkoani Pwani, inayotarajiwa kutekelezwa kwa siku 10 katika halmashauri tisa, Ulega alisema sheria haipaswi kuwa anasa kwa watu wenye uwezo wa kifedha pekee, bali haki inayopaswa kupatikana kwa kila mwananchi bila kujali kipato chake.

Alieleza kampeni hiyo imekuwa sauti ya wanyonge, wakiwemo yatima, wazee, wajane, wanawake, watu wenye ulemavu na vijana, kwa kuwawezesha kupata msaada wa kisheria unaohitajika katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Kwa mujibu wa Ulega, awamu ya kwanza ya kampeni hiyo mkoani Pwani ilifikia watu 200,243, wakiwemo wanawake 101,967 na wanaume 98,276 sawa na asilimia 9 , hali iliyochangia Rais Dkt Samia kuelekeza wizara kurejea na kuendeleza kampeni hiyo kupitia awamu ya pili.

Kadhalika amesema serikali inaandaa mpango utakaowezesha mawakili wa serikali kushughulikia mashauri ya wananchi ambayo hayana mgongano wa kimaslahi na serikali, hatua inayolenga kuongeza ushirikiano kati ya mawakili wa serikali na wa kujitegemea katika kupanua upatikanaji wa huduma za kisheria.

Ameongeza kuwa serikali imejenga mfumo wa kidijitali utakaowawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko na kufuatilia mrejesho kuhusu changamoto zao, huku ukilenga kuimarisha uratibu wa huduma za msaada wa kisheria ili zitolewe kwa wakati.

Nae Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Edwin Enosy Swalle, aliitaka serikali kuendeleza kasi ya utoaji wa huduma hizo, hasa katika maeneo ya vijijini na pembezoni ambako wananchi wako mbali na mahakama na vyombo vya maamuzi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ameishukuru serikali kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria, akisema kampeni hiyo itatoa fursa kwa wananchi kuwasilisha na kutafutiwa ufumbuzi wa migogoro ya ardhi, urithi, ukatili wa kijinsia, matunzo ya watoto na masuala ya ndoa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Ushauri ya Msaada wa Kisheria, Jaji Mstaafu Crecencia Makuru, amewataka viongozi wa wilaya na wataalamu wa sheria kuhamasisha wananchi wenye uhitaji kujitokeza kwa wingi ili wapate huduma hizo kwa haki na usawa.