Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, amesema jumla ya zabuni 430,643 zenye thamani ya Sh trilioni 42.6 zimetolewa kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST).

Kauli hiyo ameitoa Oktoba 29, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).

“Takribani asilimia 70 ya bajeti yote ya serikali inatumika kupitia ununuzi wa umma, maarufu kama tenda za serikali. Kiasi hiki kinaelekezwa kuhakikisha wazabuni wazawa na wale wa nje ya nchi wanatumia fursa hii kutekeleza miradi na kazi za serikali.

“Hivyo ni fursa ya kufanya biashara na serikali wakati umepewa dhamana ya kutoa huduma kwa maslahi ya taifa letu. NeST imejengwa na wazawa na ina matokeo makubwa na kuleta mapinduzi muhimu katika sekta ya ununuzi wa umma hapa nchini,” amesema.

Kwa sasa amesema mfumo huo unasomana na mifumo zaidi ya 30 ikiwamo ya kibenki, malipo, mifuko ya hifadhi za jamii, bodi za usajili wa wataalamu, leseni na upekuzi wa mikataba ya ununuzi.

Katika kuimarisha ufanisi na usalama wa michakato ya ununuzi wa umma, amesema wameuunganisha mfumo huo na mifumo ya kibenki ili kuhakiki dhamana za zabuni au za benki (bid securities/bank securities).

Hadi sasa, amesema mfumo huo umeunganishwa na Benki ya NMB huku TCB na CRDB ziko hatua za mwisho za kuunganishwa.

Vilevile, amesema wameanzisha mfumo (bank security portal) unaowezesha benki nyingine kutoa na kuthibitisha dhamana za zabuni kupitia NeST bila kuhitaji kuunganisha mifumo yao moja kwa moja.

Amesema mfumo huo ulioanza kutumika Oktoba Mosi, 2026 umepanua wigo wa upatikanaji wa huduma hiyo na hadi sasa zaidi ya benki 36 zimeunganishwa.

“Maboresho hayo yamerahisisha uhakiki wa dhamana za zabuni, kupunguza muda wa uchakataji na kuimarisha uwazi, usalama na ufanisi katika michakato ya ununuzi wa umma,” amesema.

Hatua hiyo, amesema imesaidia kuondoa kabisa uwezekano wa kuwa na nyaraka za kughushi katika mfumo huo na inarahisisha mchakato wa kuziwasilisha wakati wa ushiriki wa zabuni.

Kwa mujibu wa sheria ya ununuzi wa umma, amesema michakato yote ya ununuzi wa umma inatakiwa kufanyika ndani ya mfumo huo na hadi sasa tayari moduli kuu sita zimekamilika na zinaendelea kutumika na kuboreshwa kutokana na maboresho ya maoni ya watumiaji na mahitaji mapya.

Amezitaja moduli hizo kuwa ni ya usajili wa watumiaji (e-Registration), kuendesha michakato ya ununuzi (e-Tendering), malipo ya mikataba (e-Payment), usimamizi wa mikataba (e-Contract Management), katalogia (e-Catalogue) na ununuzi kupitia mnada wa kielektroniki wa kushusha bei (e-Reverse Auction).

Kupitia moduli ya usimamizi wa mikataba, amesema usimamizi wa mikataba, utayarishaji wa mkataba (contract preparation), upekuzi wa mikataba (contract vetting) hadi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na kusaini mkataba husika vinafanyika ndani ya mfumo huo.

Kando na moduli kubwa pia amezitaja ndogo ndani ya mfumo huo ikiwamo ya usimamizi wa malalamiko ya rufaa na ukaguzi na ukidhi.

Kwa upande wa moduli ya usimamizi wa malalamiko na rufaa za zabuni za umma, amesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) sasa wazabuni wenye malalamiko wanapata huduma kwa haraka kupitia mfumo huo.

“Malalamiko yao yanawasilishwa moja kwa moja na kufanyiwa kazi, kisha majibu yote yanawekwa katika mfumo kwa uwazi na haki.
Pia moduli ya ukaguzi na ukidhi imejikita kuhakikisha NeST iko salama na tunaisimamia kwa ushirikiano na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA),” amesema.

Tangu kuanza kutumika, amesema wamepata mafanikio mengi huku akiyataja machache kuwa ni kupanda kwa kiwango cha ukidhi wa sheria.

Kutokana na matumizi ya mfumo huo, amesema taasisi zimelazimika kufuata utaratibu ili kukamilisha michakato ya ununuzi na kiwango cha ukidhi wa sheria kimeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka wa fedha wa 2023/2024), asilimia 76 mwaka wa fedha wa 2024/2025) hadi kufika asilimia 79 mwaka wa fedha wa 2025/2026.

Amesema wameondokana na matumizi ya karatasi kwa sababu mfumo huo umezuia uchapishaji wa zaidi ya kurasa milioni 288.57 za nyaraka za zabuni na kuokoa Sh bilioni 27.64.

Pia amesema umewezesha utekelezaji wa upendeleo wa zabuni na bidhaa za ndani ya nchi.

“Sheria ya ununuzi wa umma imeweka upendeleo maalumu ambapo zabuni zote zenye thamani isiyozidi Sh bilioni 50 ni kwa ajili ya wazawa na imetoa upendeleo wa hadi asilimia 10 kwa wazabuni wa ndani katika zabuni zinazohusisha ushindani wa kimataifa.

“Pia umetoa upendeleo wa hadi asilimia 15 kwa bidhaa za ndani ya nchi dhidi ya bidhaa za nje. Upendeleo huu si kwa maneno tu bali kupitia NeST ni rahisi kufuatilia na kutekeleza kwani wazabuni wa nje hawawezi kubofya kitufe cha kuomba zabuni zenye thamani ya chini ya Sh bilioni 50 kwa kuwa zimewekwa kwa ajili ya wazabuni wazawa,” amesema.

Kuhusu upendeleo kwa makundi maalumu, amesema sheria ya ununuzi wa umma imezielekeza taasisi zote za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya vijana, wanawake, wazee na wenye ulemavu.

Hadi sasa, amesema makundi maalumu 33,659 yamesajiliwa katika mfumo huo na kati yao, vijana ni 16,133, wanawake 16,070, wazee 767 na watu wenye ulemavu 689.

Amesema makundi hayo yamepata zabuni zenye jumla ya Sh bilioni 82.34 na kati ya fedha hizo, vijana wamepata Sh bilioni 44.74, wanawake Sh bilioni 33.15, wazee Sh bilioni 3.78 na wenye ulemavu Sh milioni 680.21.

“Lengo la PPRA kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 [Dira 2050] ni kuwa na makundi 300,000 yaliyo tayari kuomba zabuni.

“Kutokana na nia ya kuwainua Watanzania kiuchumi, kundi maalumu linaweza kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi Sh milioni 500,” amesema.