
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein akizungumza leo, Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
********************
WAHITIMU wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, wametakiwa kuzingatia uadilifu, nidhamu na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakitoa huduma bora kwa lengo la kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohamed Shein, Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam.
Dkt. Shein amewapongeza wahitimu kwa juhudi, nidhamu na uvumilivu waliouonesha katika safari yao ya kitaaluma, akisisitiza kuwa wanapaswa kutumia maarifa na ujuzi walioupata chuoni kwa manufaa ya jamii.
Amesema mahafali hayo ni fursa ya kutambua mafanikio ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kuimarisha ubora wa elimu, kukuza ubunifu na kupanua fursa za elimu ya juu nchini.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amesema utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tano wa chuo hicho umefikia wastani wa asilimia 89.58, hatua inayoonesha maendeleo katika utekelezaji wa mipango ya taasisi hiyo.
Amesema mafanikio hayo yanaenda sambamba na juhudi za kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika kampasi mbalimbali za chuo hicho ili kuimarisha mazingira ya utoaji elimu bora.
Prof. Mwegoha amesema Ndaki ya Dar es Salaam inaendelea na maandalizi ya programu nne mpya za masomo ya juu, zikiwemo programu mbili za Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Usimamizi wa Biashara na Utawala Bora na Uongozi.
Programu nyingine mbili ni za Stashahada ya Uzamili (Postgraduate Diploma) katika Usimamizi wa Biashara na Utawala wa Umma.
Amesema programu hizo zinalenga kupanua fursa za mafunzo ya juu na kuimarisha uwezo wa chuo katika kuzalisha wataalamu wenye maarifa na ujuzi unaohitajika katika maeneo ya uongozi, usimamizi na utawala.
“Maandalizi haya yanalenga kupanua fursa za mafunzo ya juu na kuimarisha uwezo wa Chuo katika kuzalisha wataalamu wenye maarifa na ujuzi unaohitajika katika uongozi, usimamizi na utawala. Inatarajiwa kuwa programu hizi zitaanza kutolewa katika mwaka ujao wa masomo baada ya kukamilika kwa taratibu za ithibati,” amesema Prof. Mwegoha.
Katika eneo la utafiti na huduma za kitaalamu, amesema wanataaluma wa Ndaki ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na wenzao wa Kampasi Kuu wameshiriki katika miradi minne ya utafiti na kuendesha kozi fupi kwa taasisi mbalimbali.
Aidha, amesema chuo hicho kwa kushirikiana na Kuhne Foundation kiliandaa Kongamano la Nane la Kimataifa la Usimamizi wa Uendeshaji na Mnyororo wa Ugavi Barani Afrika (ACOSCM), lililowakutanisha washiriki kutoka Afrika na Ulaya.
Amesema ushirikiano huo umechangia kuimarisha nafasi ya Chuo Kikuu Mzumbe katika utafiti na mijadala ya kitaaluma ya kimataifa, huku chuo kikiendelea kutumia utaalamu wa watumishi wake kutoa mafunzo na huduma za ushauri zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali.
Prof. Mwegoha amewataka wahitimu kuendelea kujifunza na kuendana na mabadiliko ya teknolojia, hususan matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwemo Akili Mnemba (AI), katika kutekeleza majukumu yao.
Amesisitiza kuwa wahitimu wanapaswa kutumia elimu na ujuzi walioupata kuwanufaisha wengine na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Balozi Modest Jonathan Mero, amewataka wahitimu kuzingatia nidhamu na kutumia elimu waliyoipata kwa ufanisi wanapoingia katika soko la ajira au kuamua kujiajiri.
Amesema wahitimu wanapaswa kuwa wabunifu na kutumia maarifa yao kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazowawezesha kujipatia kipato na kutengeneza fursa za ajira kwa watu wengine.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Mhitimu Bora wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, kwa mwaka 2026, Enoishi Kimirei, amewashukuru viongozi wa chuo, wahadhiri na watumishi kwa mchango wao katika kuwawezesha kufikia hatua hiyo muhimu ya maisha yao.
Pia amewashukuru wazazi na walezi kwa msaada, ushauri na uvumilivu waliouonesha katika kipindi chote cha masomo yao.
Mahafali hayo yamewakutanisha viongozi wa chuo, wanataaluma, wahitimu, wazazi, walezi na wageni waalikwa katika kusherehekea mafanikio ya wahitimu wa mwaka wa masomo 2025/2026.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha akizungumza leo, Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Balozi Modest Jonathan Mero, akizungumza leo, Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
Mlau wa Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Elizabeth Lulu Genda akitoa nasaha kwa wahitimu wakati wa Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam yaliyofanyika tarehe 29 Oktoba 2026, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Dar es Salaam
Rasi wa Ndaki ya Dar es Salaam Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Cyriacus Binamungu akizungumza leo, Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein (kulia) akimkabidhi zawadi Mhitimu Bora wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, kwa mwaka 2026, Enoishi Kimirei,




