Na MWANDISHI WETU

CHAMA Cha Wataalamu wa Kuchunguza Udanganyifu na Wizi wa Fedha (ACFE), kimeanda mkutano wa sita wa mwaka wa Mapambano dhidi ya Udanganyifu, utakaofanyika Novemba 16 hadi 20, mwaka huu Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).

Mkutano huo utafanyika sambamba na Maadhimisho ya Kimataifa ya Wiki ya Mapambano dhidi ya Udanganyifu Duniani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ACFE, Abduel Kelakela alisema wameandaa mkutano huo ili kutoa elimu na kuwajengea uwezo wadau mbalimbali kuhusu mapambano dhidi ya udanganyifu.

Alisema katika maendeleo ya teknolojia yameleta fursa kubwa kwa uchumi na utoaji huduma, wakati huo huo yameibua mbinu mpya za udanganyifu zinazohitaji taasisi na wananchi kuwa na ulelewa, mifumo na uwezo wa kukabiliana nazo.

Alisisitiza mkutano huo utatoa jukwaa la kujadili namna ya kuzuia, kubaini na kuchunguza udanganyifu ikiwemo kuimarisha maadili, uwajibikaji na kutumia teknolojia ya uchambuzi wa takwimu katika kusimamia hatari za udanganyifu.

Alisema katika mkutano huo wenye kauli mbiu ‘Kujenga Upya Mikakati ya Usimamizi wa Vihatarishi vya Udanganyifu kwa Taasisi Imara katika Enzi ya Akili Unde, Takwimu na Fedha za Kidijali’, utahusisha majadiliano mapana ya udanganyifu katika huduma za kifedha za kidijitali, manunuzi na maeneo mengine ya uwendeshaji wa taasisi.

“Tunatarajia kuwakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, wakaguzi, wachunguzi, wataalamu wa udhibiti na taasisi za habari, vyombo vya utekelezaji wa sheria, wataalamu wa sekta ya fedha na wadau wengine.

“Ushirikiano huo ni muhimu katika kujenga taassi imara na kulinda rasilimali za umma na sekta binafasi.

“Tunatoa shukrani zetu kwa Wizara ya Fedha, kupitia Mkaguzi wa Ndani wa Serikali na Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar kwa kukubali kuwa washirika wa kimkakati katika mkutano huo,” alisema Kelakela.

Awali, Mkuu wa Divisheni ya Mifumo ya Kiutawala na Maslahi, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Zanzibar, Khadija Ali Hassan alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa na muhimu katika kuelimisha jamii na kuhamasisha uadilifu na uwajibikaji.

“Tunaomba muendelee kushirikiana nasi katika kuhamasisha wananchi na taasisi kuchukua hatia dhidi ya udanganyifu kwani una gharama kubwa na unarudisha nyuma maendeleo.

“Hii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Marais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kupambana na udanganyifu na kuchangia kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema Khadija.

Kwa mujibu wa ripoti ya ACFE, makampuni duniani hupoteza asilimia tano ya mapato yote kila mwaka kutokana na udanganyifu.