Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

MWENYEKITI wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kibaha, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Fadhil Emmanuel Nkurlu, ameifungia shule binafsi ya sekondari ya Katorosia, iliyopo Kata ya Pangani mkoani Pwani, kutokana na kukosa vigezo vinavyotakiwa pamoja na kukaidi maagizo ya serikali yaliyotolewa Julai 25, 2025.

Shule hiyo ilielekezwa kufungwa kutokana na mazingira hatarishi na yasiyoridhisha kwa wanafunzi kuishi, ikiwemo hali mbaya ya mabweni, uchafu wa vyoo na maeneo ya kulala, vitanda vibovu pamoja na majengo chakavu.

Aidha, shule hiyo iliyosajiliwa kutoa elimu ya kutwa, imebainika kuwa mmiliki alikuwa akilaza wanafunzi shuleni, huku wanafunzi wa kike na wa kiume wakilala katika mabweni yaliyotajwa kutokuwa na mazingira salama na yanayokidhi mahitaji ya wanafunzi.

Nkurlu alifanya ziara ya kufunga shule hiyo November 2,2026 akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na maofisa Idara ya Elimu Sekondari ya Manispaa ya Kibaha.

Akizungumza wakati wa hatua hiyo, Nkurlu alisema shule hiyo imekiuka na kukaidi maagizo ya serikali pamoja na maelekezo ya Udhibiti Ubora wa Shule, licha ya kupewa muda wa kufanya marekebisho.

Alisema maagizo hayo si mapya wala ya dharura, hivyo mmiliki alipaswa kuyatekeleza na kuhakikisha wanafunzi hawaendelei kuwepo shuleni.

Aliongeza kuwa kufungwa kwa shule hiyo ni salamu kwa wamiliki wengine wa shule wanaokiuka taratibu, miongozo na maelekezo ya sekta ya elimu, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kufanya hivyo.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kibaha , Theresia Charles alisema shule hiyo ilisimamishwa usajili mwaka 2025 kutokana na kukosa sifa za kudahili wanafunzi.

Alisema pia shule hiyo imekuwa na changamoto za utoaji wa elimu, ikiwemo walimu kutotoa majaribio ya mitihani na kutofundisha wanafunzi ipasavyo.

Alieleza kuwa madai ya mmiliki kuwa shule imefungwa tangu Ijumaa iliyopita hayana msingi, kwa kuwa shule nyingine hazijafungwa na hakuna sababu ya shule hiyo kusitisha shughuli zake kabla ya muda.

Naye Mtendaji wa Mtaa wa Mtakuja, Evena Michael, alisema mmiliki wa shule hiyo amekuwa mkaidi, akieleza kuwa licha ya viongozi kutoa maelekezo, alikuwa akiendelea na shughuli zake mara baada ya viongozi kuondoka.

Alisema mazingira ya shule hiyo hayakuwa salama kwa wanafunzi kusomea na kuishi, hivyo hatua ya kuifunga ilikuwa muhimu kwa ajili ya kulinda usalama na afya za wanafunzi.

Kwa upande wake, mmiliki wa shule hiyo, Emalieza Sekwao Chilemeji, alisema shule hiyo ilianza mwaka 2013 na kusajiliwa kama shule ya kutwa, huku akikiri kukiuka maagizo ya serikali kuhusu mazingira ya shule na afya za wanafunzi, pamoja na kuigeuza kuwa shule ya bweni.

Chilemeji alisema amepokea maagizo yaliyotolewa na serikali na kuahidi kutoruhusu mwanafunzi yeyote kuendelea kuwepo shuleni kuanzia sasa.