*Hekta 617, majengo 26 ya wizara na 11 ya taasisi za Serikali kuhudumia watumishi 18,510 Mtumba

*Uwekezaji wa takribani Sh bilioni 700 wafungua ukurasa mpya wa utawala, uchumi na maendeleo ya Dodoma

*Ndoto ya mwaka 1973 yapitia awamu mbalimbali za uongozi hadi kufikia hatua kubwa ya Mji wa Serikali

Doto Kwilasa na Joel Mjengi, JamhuriMedia, Dodoma

Katika eneo lenye ukubwa wa takribani hekta 617, sawa na zaidi ya mita za mraba milioni sita, jijini Dodoma, Tanzania imejenga kitovu kipya cha shughuli za serikali kitakachobadili namna wizara na taasisi zake zinavyofanya kazi, kuwasiliana na kuhudumia wananchi; JAMHURI linaripoti.

Ni Mji wa Serikali Mtumba, eneo lenye majengo makubwa ya kisasa, mtandao wa barabara za lami, mifumo ya mawasiliano, umeme na huduma nyingine, lililopangwa kukusanya shughuli za wizara na taasisi mbalimbali katika sehemu moja.

Tofauti na utaratibu wa zamani wa kuwa na ofisi za serikali zilizotawanyika katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Mtumba inaleta mfumo wa kuzikutanisha taasisi hizo katika eneo maalumu, hatua inayotarajiwa kurahisisha uratibu wa shughuli za serikali na kuongeza ufanisi wa utendaji.

Kwa ukubwa wa eneo, idadi ya majengo, miundombinu na shughuli zinazokusudiwa kufanyika humo, Mtumba inajitokeza kama jiji ndani ya jiji, lenye nafasi ya kuwa kitovu cha utawala na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayolizunguka.

Uzinduzi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, Oktoba 30, 2026, umefungua ukurasa mpya katika safari ya zaidi ya nusu karne ya kuhamishia makao makuu ya nchi kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Na sasa, uwekezaji wa takribani Sh bilioni 700 unatarajiwa kubadili utendaji wa serikali na utoaji huduma kwa Watanzania.

Serikali chini ya eneo moja

Katika hatua iliyozinduliwa, Mtumba ina majengo 26 ya wizara na majengo 11 ya taasisi za serikali, yenye uwezo uliotajwa wa kuhudumia watumishi wapatao 18,510.

Idadi hiyo inaonyesha ukubwa wa shughuli zinazotarajiwa kuendeshwa katika eneo hilo, ambalo pia lina miundombinu inayounganisha ofisi mbalimbali na kurahisisha mawasiliano kati ya taasisi.

Kwa miaka mingi, shughuli za serikali zilikuwa zikiendeshwa kutoka katika majengo yaliyotawanyika sehemu mbalimbali za Dar es Salaam, hali iliyohitaji watumishi kusafiri kutoka ofisi moja kwenda nyingine kwa ajili ya mikutano, mawasiliano na uratibu wa majukumu.

Ujenzi wa Mtumba unapunguza changamoto hizo kwa kuzikutanisha wizara na taasisi nyingi katika eneo moja, ambako mawasiliano na ushirikiano wa kiutendaji vinafanyika kwa urahisi zaidi.

KWA HABARI ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA NOVEMBA 3- 9, 2026