* Dereva bodaboda kwa sasa anapata Sh 75,000 kwa siku badala ya Sh 15,000

*Wateja wa baba lishe waongezeka kwa siku hadi kufikia zaidi ya 100 kutoka 20

Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Mtwara

Maboresho yaliyofanyika Bandari ya Mtwara yameanza kuleta manufaa kwa wananchi wanaoizunguka huku makundi ya wajasiriamali na wafanyakazi wadogo yakishuhudia kuongezeka kwa fursa za kibiashara na vipato binafsi.

Baba lishe, mama lishe, madereva, bodaboda na makuli ni miongoni mwa wanufaika wanaosema shughuli zao zimeimarika kutokana na ongezeko la shughuli za bandari hiyo baada ya kuboreshwa kwa gharama ya Sh bilioni 157.8 na Desemba 31, 2020 ikaendelea na kazi kwa kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo na kufikia tani milioni 2.6 kwa mwaka kutoka tani 400,000 na hatua hiyo inawapa wateja wengi zaidi na kusaidia mapato yao kukua ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Watoa ushuhuda

Wakizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalumu yaliyofanyika kwa nyakati tofauti hivi karibuni pembezoni mwa bandari hiyo, wanaelezea ukuaji wa shughuli za bandari ulivyobadilisha shughuli zao na kufungua fursa mpya za kujiongezea kipato.

Mfanyakazi wa Idara ya Zimamoto wa Bandari ya Mtwara, Irene Nguli, anasema uwekezaji na uendeshaji umewanufaisha vijana kwa kupata ajira za kudumu na kazi za msimu kutokana na usafirishaji wa shehena za korosho, mbaazi, ufuta, magari na saruji kutoka Kampuni ya Dangote.

Pia anasema biashara na huduma ndogondogo zimeongezeka kwa sasa kutokana na ongezeko la watu bandarini kwa kusaidia biashara ya usafirishaji na madereva wa bodaboda wanajipatia vipato vyao vya kila siku.

“Huduma ya chakula kwa baba lishe na mama lishe imeongezeka na kujiongezea vipato vyao vya kila siku. Kitu kingine, imepunguza uhalifu mitaani kwa sababu vijana wengi wa Mtwara sasa hivi wanafanya kazi humu bandarini.

“Nashauri vijana wenzangu tujitahidi kuongeza ujuzi kutokana na kazi zinazoendelea bandarini ili tupate ajira. Kwa upande wangu nimenufaika kutokana na kazi yangu inaniongezea kipato cha kuendesha maisha yangu ya kila siku na familia yangu,” anasema.

Anaishukuru bandari hiyo kuwajali vijana na kuwapatia ajira kwa kusema: “Kabla ya hapa nilikuwa na ujuzi wa zimamoto ndiyo maana nikapata kazi hapa bandarini. Ushauri wangu kwa vijana wenzangu tukimbilie fursa hapa zipo nyingi kutokana na usafirishaji. Kwa sababu sehemu yoyote yenye uwekezaji lazima kuna huduma za jamii zinahitajika.

“Wenye ujuzi wasikae nyumbani, waje bandarini kuomba kazi. Hata kama ni vibarua au kazi za msimu zipo zinapatikana kwa sababu bandari imeshaanza kushusha meli za magari na wanahitajika madereva, makarani na watu wa kuegesha magari bandarini.”

Mfanyakazi wa Idara ya Zimamoto wa Bandari ya Mtwara, Irene Nguli

Anawataka vijana wenzake wawe waaminifu kwa waajiri kwa sababu hiyo ni silaha muhimu kwa mustakabali wa maisha yao.

“Waajiri ni waaminifu kwetu nasi tuwe waaminifu kwao. Uaminifu kazini ni silaha ya kukutoa nafasi fulani kwenda nyingine,” anasema.

Dereva wa Dangote, Rashidi Harouni, anasema kwa sasa kuna manufaa makubwa baada ya gati namba nne kuboreshwa kwa kurahisisha huduma za usafirishaji.

“Mfano sisi tunapakia saruji kutoka kiwandani na kuileta hapa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Msumbiji, Comoro na Zanzibar na inatusaidia kwa haraka kwa sababu ikifika hapa inapakiwa moja kwa moja na kuondoka.

“Baada ya maboresho ya hili gati uchukuzi umerahisishwa kwa sababu sasa hivi magari mengi yanashukia hapa bandarini Mtwara, kwa hiyo hata vijana tumepata fursa ya kuchukua magari na kuyapeleka nchi za jirani,” anasema.

Pia anasema kuna faida kubwa kupitia maboresho hayo kwa kuwa yameokoa muda ikilinganishwa na zamani kwa mwezi mmoja inaweza ikaja meli moja au mbili kushusha mzigo lakini sasa hivi ndani ya wiki moja zinakuja meli sita hadi saba kushusha mzigo.

“Ujumbe kwa vijana wenzangu hapa bandarini ni sehemu inayotupa riziki, tukija hapa tuithamini bandari na tuwe waaminifu kwa sababu kuna mtu anapewa gari alipeleke Rwanda au Burundi lakini akifika njiani anaanza kung’oa vifaa na kuviuza.

Dereva wa Dangote, Rashidi Harouni

“Kitendo hicho kinapoteza uaminifu na kusababisha kukosa hizo fursa. Bandari hii itakuwa kuja kuwa bora zaidi kwa sababu inaboreshwa kwa kasi. Ushauri wangu tuendelee kuwa waaminifu na kuitangaza kwa wengine kwamba iko vizuri,” anasema.

Baba lishe wa mgahawa wa Bandari ya Mtwara, Benjamin Lutende, anaishukuru serikali kwa maboresho waliyoyafanya bandarini hapo kwa sababu yameleta mafanikio kwao na wateja wanaonunua chakula na vinywaji wameongezeka.

“Sasa hivi saruji, korosho, makaa ya mawe yanasafirishwa hapa bandarini na tunapata wateja wengi na sisi kama watoa huduma ya chakula na vinywaji tumenufaika,” anasema.

Wateja anasema wameongezeka, na kwa wastani kwa siku wanawapata zaidi ya 100 wakati zamani waliwapata kati ya 20 au 25.

“Zamani hali haikuwa nzuri kwa sababu tulitegemea tuuze chakula na vinywaji kwa watumishi wa bandari peke yao. Tunawaomba wateja waendelee kuitumia hii bandari na kuja kwao kunatunufaisha sisi watoa huduma za chakula,” anasema na kuongeza:

“Tunawakaribisha kuja hapa kula chakula chetu ni kizuri. Watumiaji wa bandari waendelee kuitumia kwa manufaa ya nchi ila nashauri tuboreshe mazingira yake ili iendelee kuvutia waliopo nje ya Mtwara.

“Wateja wengine waje kuitumia hata wale wa nchi za jirani kama Msumbiji kwa sababu bandari yetu imekuwa bora na hata mizigo yao inaweza kupitia hapa.”

Baba lishe wa mgahawa wa Bandari ya Mtwara, Benjamin Lutende

Mwenyekiti wa Bodaboda Kijiwe cha Mti Pesa, Abdala Kasuku, anasema kwa sasa wana faidika kwa kiwango kikubwa kutokana na maboresho ya bandari hiyo.

“Tunapata wageni wa kuwasafirisha maeneo mbalimbali hapa mjini pindi meli zinapokuja kushusha mizigo. Sisi kama bodaboda hasa msimu wa korosho hapa tunapiga kazi mwanzo mwisho, ukija kazini na pikipiki yako unaanza kupakia abiria.

“Kuna vijana wanafanya huko ndani bandarini, hapa kuna meli za saruji, korosho na tangu maboresho yafanyike kwa kweli tunashukuru mambo yanakwenda vizuri na ikiwezekana wateja wengine wa Malawi, Zambia na Msumbiji waje kuitumia hii bandari ili sisi tufaidike zaidi,” anasema.

Pia anasema ana uzoefu wa kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 12 na anasomesha watoto wake hadi elimu ya chuo kikuu na sasa hivi anajenga nyumba ya kuishi na familia yake.

Anasema wanatarajia kupokea wageni wengi kutoka mikoa mbalimbali wanaokuja kufanya kazi kutokana na fursa zilizopo bandarini.

“Ushauri wangu, tushirikiane kufanya kazi kwa pamoja. Jingine, wateja wengine waje kushusha mizigo yao hapa. Lugha si tatizo kwa wageni kutoka nje ya nchi hasa kwa wanaotoka Zambia na Madagascar, tunaongea nao Kiingereza na tunaelewana.

“Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan aendelee kuiboresha hii bandari na sisi vijana atushike mkono. Ni kweli madereva bodaboda japo si wote wanaendesha pikipiki kwa fujo bila kufuata sheria za usalama barabarani. Hizi ndizo changamoto za kazi zetu na tunawashauri waache,” anasema.

Anawashauri bodaboda wenzake kuifanya kazi hiyo kwa kuithamini na waione ni sehemu ya maisha yao. Pia anawaomba wateja wengi waende hata kama msimu wa korosho utakwisha.

Katika hatua nyingine, anasema kwa sasa anapata hadi Sh 75,000 kwa siku wakati zamani kabla ya maboresho ya bandari hiyo alipata kati ya Sh 15,000 hadi Sh 25,000.

Gabriel Jarome anayefanya shughuli za ubaharia bandarini hapo, anasema binafsi ananufaika na maboresho hayo kwa kujipatia kipato na kujuana na watu wanaomsaidia kupata fursa mbalimbali.

“Kwa mfano kuna wageni wengi wanakuja na sasa hivi tunapokea meli za magari, ina maana kupitia kitengo changu cha ubaharia napata fursa ya kuonana na mawakala wa meli walioagiza magari na kuzungumza nao na kupata fursa ya kufanya nao kazi,” anasema.

Vilevile anasema wanajifunza mambo mbalimbali, mathalani kuna mtu yuko kitengo cha kuendesha mitambo lakini akija anaweza akawa kitengo cha ubaharia cha kufunga na kufungua meli au kingine na akaendelea kujifunza na akafanya kazi nyingine.

“Tunajifunza huku tunajipatia fedha na tunajuana na watu mbalimbali. Nawashauri vijana tufuatilie fursa kwa sababu haikufuati nyumbani bali inatafutwa.

“Tunapoingia bandarini kutafuta riziki basi tufanye kazi iliyotuleta, tena kwa bidii, uaminifu na tujitume na fursa zitakuja tu, lakini ukija bandarini haujitumi na hautafuti fursa zingine hauwezi kuzipata japo zipo,” anasema.

Kuhusu uaminifu, anasema sehemu yoyote ile ni kitu muhimu kwa binadamu na unapokuwa mwaminifu unajihakikishia kubaki kazini.

“Nawaomba vijana wenzangu tuwe waaminifu, tutafika mbali, lakini kijana ukiwa mdokozi, unachukua vifaa vya magari ya wateja, ukikamatwa utazuiliwa kuingia bandarini, utazikosa fursa. Pia mtu mwingine akipata taarifa zako hawezi tena kukupa kazi.

“Hapa kuna vitengo tofauti vya ubaharia, operesheni, uhandisi, madereva wa magari yanayokwenda nchi jirani, wapo mafundi, mabaharia. Fursa ni nyingi na unaweza kuja na fani ya udereva na ikikupendeza ukawa mwendesha mitambo na kuhamia kwingine kutokana na uaminifu wako,” anasema.

Anamuomba Rais Samia aendelee kuboresha bandari ili fursa ziendelee kupatikana. Pia anawashauri vijana wenzake wafanye kazi, wajitume na watafute kazi si za bandarini tu bali wajaribu maeneo mengine kuliko kukata tamaa na kukaa nyumbani kwa sababu wao ndio nguvu kazi ya uchumi wa nchi.