Na Mwandishi Maalumu

WATAALAM wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Stanford Health Care, Stanford University ya nchini Marekani, wanaendesha kambi maalumu ya tiba mionzi inayolenga kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu katika maeneo mbalimbali ya tiba hiyo.

Mafunzo hayo yanahusisha madaktari bingwa wa saratani (Clinical Oncologists), wataalamu wa tiba mionzi (Radiotherapists/Medical Dosimetrists) wafizikia tiba (Medical Physicists) na wauguzi bingwa wa saratani (Oncology Nurses).

Kambi hiyo ya siku 14 ambayo imeanza leo inatarajiwa kuwahudumia wagonjwa zaidi ya 100. Katika kipindi hicho wataalamu kutoka taasisi hizo mbili watashirikiana kutoa huduma za matibabu, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ujuzi wa kutumia mbinu za kisasa za tiba mionzi, zikiwemo Intensity-Modulated Radiation Therapy (IMRT), Volumetric Modulated Arc Therapy (VMAT) na Stereotactic Body Radiation Therapy (SBRT).

Akizungumza wakati wa kuwapokea wataalamu hao kutoka Marekani Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo alisema mafunzo yatakayotolewa kwenye kambi hiyo ni muhimu kwa kuwa yatawasaidia wataalamu kuongeza ujuzi na utaalamu katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi wa tiba mionzi.

Dkt. Msemo ambaye pia ni Daktari Bingwa na Mbobezi wa Magonjwa ya Saratani na Tiba Shufaa alisema kambi hiyo ni fursa muhimu kwa wataalamu wa ORCI kujifunza na kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali ya tiba mionzi hatua itakayochangia kuboresha huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo.

“Nikiwa kama Daktari Bingwa na Mbobezi wa Magonjwa ya Saratani nitahudhuria mafunzo haya ambayo ni muhimu katika kazi yangu ya kutibu wagonjwa kwani yatanisaidia kuongeza ujuzi na kutoa huduma bora zaidi,” alisema Dkt. Msemo.
Aliwakaribisha wataalamu hao nchini Tanzania na kueleza matumaini yake kuwa katika kipindi watakachokuwa nchini watafurahia mazingira ya Tanzania, kujifunza lugha ya Kiswahili na kupata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Fizikia Tiba (Medical Physicist) kutoka Stanford Health Care, Stanford University, Piotr Dubrowski alisema ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo unatoa fursa kwa wataalamu wa pande zote mbili kubadilishana uzoefu, kufahamu utaalamu uliopo ORCI na kutambua maeneo yanayoweza kuimarishwa kupitia mafunzo na kufanya kazi kwa pamoja.

Alisema ushirikiano huo utawasaidia wataalamu kuelewa mahitaji yaliyopo katika utoaji wa huduma za tiba mionzi na kuweka mikakati ya pamoja itakayochangia kuboresha matibabu kwa wagonjwa wa saratani.

“Tutashirikiana kufanya kazi pamoja katika kuwatibu wagonjwa wa saratani wanaohitaji huduma za tiba mionzi. Ili kupata matokeo mazuri tunahitaji kufahamu mahitaji ya wataalamu wenzetu. Hilo litatusaidia kujenga ushirikiano utakaowezesha kuimarisha huduma,” alisema.

Naye Mratibu wa kambi hiyo ambaye pia ni Mtaalamu Mwandamizi wa Tiba Mionzi wa ORCI, Mpanda Mngoya alisema kambi hiyo inalenga kujengeana uwezo na kuimarisha utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ikiwemo matumizi ya mbinu ya Stereotactic Body Radiation Therapy (SBRT).

Alisema kambi hiyo pia itawajengea uwezo wataalamu kutoa huduma ya Total Skin Electron Beam Therapy (TSEBT) ambayo hutumia mionzi ya elektroni kutibu saratani inayoathiri sehemu kubwa ya ngozi au ngozi ya mwili mzima, kama ilivyo kwa ugonjwa wa Mycosis Fungoides.

Katika utoaji wa huduma za tiba mionzi (Radiotherapy) wataalamu hao watatumia mitambo na vifaa vya kisasa vya uchunguzi vilivyopo ORCI ikiwemo CT Scan, MRI na PET-CT Scan ili kusaidia katika maandalizi na utoaji wa matibabu kwa wagonjwa.

1000515187
1000515193