Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

WANANCHI Tangini, Mailmoja na Pangani, Manispaa ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, wamesema Kampeni ya Samia Legal Aid imekuwa mkombozi kwao kwa kuwasogezea huduma za kisheria karibu na maeneo yao, ambazo awali walishindwa kuzimudu kutokana na gharama za usafiri na huduma hizo.

Wakizungumza wakati wa kampeni hiyo inayofanyika katika kata hizo akiwemo Ally Mshamu, Fatuma Ismail, Mama Ikram na Seif Salim, walisema upatikanaji wa huduma za RITA, msaada wa mawakili na wanasheria umewapa nafasi ya kupata ushauri na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizokuwa zikikwamisha maisha yao.

Salim alifafanua kuwa wengi wao walikuwa wakikabiliwa na changamoto za kisheria lakini wakishindwa kufuata taratibu za kupata haki kutokana na gharama za kufika kwenye taasisi husika, hali iliyosababisha baadhi ya migogoro kuendelea kwa muda mrefu.

Fatuma aliipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo, akisema imewapa fursa ya kupata msaada wa kisheria bila kikwazo cha gharama, huku akiwahimiza wananchi wengine kujitokeza kutumia huduma hizo kabla wataalamu hawajarejea maofisini na kuwalazimu kuanza tena kuhangaika kutafuta nauli.

Timu ya wataalamu kupitia Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid), Manispaa ya Kibaha, inayoongozwa na Wakili Revocatus Thadeo Mathew, inaendelea kutoa huduma hizo kwa wananchi kwa kutembelea kata mbalimbali.

Revocatus alisema hadi Novemba 5, mwaka huu, kampeni hiyo ilikuwa imefikia siku ya nane kati ya 10, huku akishukuru wananchi kwa kujitokeza kupata huduma na ushauri, hususan kuhusu masuala ya ndoa, ardhi, mirathi na migogoro ya kifamilia.

Alisema wataalamu wamekuwa wakiwapatia wananchi elimu na ushauri wa kisheria ili kuwasaidia kuelewa taratibu za kutafuta haki na kupata ufumbuzi wa migogoro yao kwa mujibu wa sheria.

“Wananchi waendelee kujitokeza kutumia fursa hii kutoa taarifa za changamoto zinazowakabili na kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa sheria ili kupata ufumbuzi wa migogoro yao kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo,” alisema.

Mratibu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid), Wakili Innocent Magesa, alisema maelfu ya wananchi wamejitokeza katika kata, halmashauri na wilaya mbalimbali kutoa madukuduku yao na kupata msaada wa kisheria.

Magesa alifafanua kuwa kampeni ya Samia Legal Aid awamu ya pili katika Mkoa wa Pwani inatekelezwa katika halmashauri tisa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa haki na kuhakikisha wananchi wenye uwezo mdogo wa kiuchumi wanapata huduma za kisheria.

Alisema kampeni hiyo ilianza Oktoba 29, mwaka huu, na inatarajiwa kuhitimishwa Novemba 7, 2026, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwapatia elimu, ushauri na msaada wa kisheria katika maeneo yao.